Suleiman Msuya
Paul Makonda |
UAMUZI wa vyombo vya habari kumsusia Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda kufanya naye kazi kumepongezwa na wadau.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati tofauti jana, wadau
wa habari nchini walisema uamuzi huo umechelewa na kushauri kuwa ungehusu
Serikali nzima kwa wanachodai kuwa anapewa kiburi na wakubwa zake.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya
Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema kwa mtazamo wake anapongeza hatua hiyo,
huku akisisitiza kuwa ingekuwa vema kutofanya kazi na Serikali nzima.
Sugu alisema kwa welewa wa kawaida inaonesha dhahiri
anachofanya Makonda ni maagizo ya wakubwa wake wa kazi hivyo hakuna sababu ya
kufanya kazi nao wote.
“Makonda ni sawa kutoandikwa ila naamini anachofanya si
kwa uamuziwake, kuna watu wanamtuma ambao ndio wamempa nafasi hiyo inapaswa nao
wasiandikwe,” alisema.
Mbunge huyo alisema haiwezekani Makonda kuchukua askari
wote aliokwenda nao katika televisheni ya Clouds Media bila mkuu wake kuhusika,
hivyo itakuwa vema nao kutoandikwa.
Alisema katika ulimwengu huu wa sasa ambao demokrasia
inatakiwa kutamalaki, haingii akilini kuona tukio kama alilofanya Makonda
likichekewa kwani linaweza kusababisha jamii kupotoka.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC),
Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema uamuzi huo ni wakuungwa mkono na watu huo ili
kuhakikisha kuwa mamlaka husika zikichukua hatua.
Dk Bisimba alisema pia angependa kuona zikiwepo hatua
nyingine za kisheria kama kwenda mahakamani ili kuhakikisha kuwa haki
inatamalaki nchini kwa watu wote.
Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema uamuzi wa
vyombo vya habari ungepaswa kufanyika tangu kupitishwa Sheria ya Huduma kwa
Vyombo vya Habari ambayo ililalamikiwa na jamii nzima.
Alisema anachofanya Makonda ni kosa kisheria na hakiwezi
kuvumiliwa na mtu yeyote na kwamba kila kona inalalamika kwa Serikali kushindwa
kusimamia haki.
“Vyombo vya habari vimechelewa sana kuchukua uamuzi huu
kwani wangepaswa kufanya hivyo katika mchakato wa sheria yenu ambayo
imepitishwa hivi karibuni,” alisema.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu CCM, Daniel
Zenda alisema haungi mkono uamuzi wa vyombo vya habari kutoandika habari za
kikazi zinazomhusu Makonda na kwamba anaamini kuwa ni kutowatendea haki
wananchi.
Alisema ni vema uamuzi huo ukawa ni kuzuia habari zake
binafsi ili wananchi waweze kujua nini kinachoendelea katika mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment