Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekuwa na `wakati
mgumu’ akihusishwa na matukio yanayoibua mjadala kwenye jamii, kiasi cha kuwapo
hisia za kutumia vibaya madaraka yake, hivyo anastahili ‘kupumzishwa’.
Yapo matukio mengi katika orodha yake yaliyofanywa ama kumhusisha
Makonda. Si rahisi kuyataja yote kwa uhalisia wake yakatosha kwenye safu hii.
Haiwezekani. Kwamba katika ujumla wake yanaibua hisia za watu ‘kumchoka’,
wakitaka awajibike ama kuwajibishwa.
Rais John Magufuli akizungumza jana katika hafla kuweka jiwe la msingi
ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Mandela na Morogoro,
eneo la Ubungo, akagusia hisia za wananchi hususani wakazi wa jijini Dar es
Salaam kumhusu Makonda.
Akasema yapo mambo mengi yanayozungumzwa na watu kumhusu Makonda,
akiyaunganisha kuwa miongoni mwa hulka ya kujadili mambo binafsi badala ya
masuala ya maendeleo, ambayo binafsi (Rais Magufuli) anaamini kuwa ndio msingi
wa maendeleo.
Ni kweli, haiwezekani kupata maendeleo yaliyo endelevu kama
wananchi ‘watakalia’ kuwajadili watu badala ya masuala. Pamoja na ukweli huo,
lipo tukio moja ambalo hadi sasa linaweza kutajwa kuwa kilele cha yale
yanayohusishwa na Makonda. Uvamizi wa studio za kituo cha redio na runinga cha
Clouds cha jijini Dar es Salaam, akiwa na askari wenye silaha za moto.
Ni tukio linalodaiwa kutokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kuibua
taharuki kwa viongozi na wafanyakazi wa kampuni hiyo ya habari, na baadaye umma
mpana kufuatia kusambaa kwake kupitia mitandao ya kijamii.
Viongozi wa Clouds wameshalizungumzia na kuthibitisha kutokea kwa
tukio hilo, taarifa imeshawasilishwa polisi na viongozi kadhaa akiwamo Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amelitembelea eneo la tukio
na kuunda timu ya uchunguzi ya watu watano inayotarajia kutoa ripoti yake leo.
Wakati hali ikiwa hivyo, Rais Magufuli amemtaka Makonda kuendelea
‘kuchapa kazi’ na kwamba rai ya baadhi ya watu kumtaka amuwajibishe kwa
kumuondoa kwenye nafasi hiyo, haiwezekani kwa vile hafanyi kazi kwa kuelekezwa na
mtu, isipokuwa kufanya uamuzi pale inapofaa.
Hivyo inaweza kutafsiriwa kwamba Makonda amepata uhakika wa kuendelea
kudumu katika utumishi wa umma akiwa Mkuu wa Mkoa, kwa maana ukweli unabaki kuwa
hakuna shinikizo lolote linaloweza kumuondoa katika nafasi hiyo isipokuwa
kupitia mamlaka za uteuzi ambazo zipo kwa Rais.
Pamoja na ukweli huo, ni wazi kwamba tukio la kuzivamia studio za
Clouds unaomhusisha Makonda, mmoja wa viongozi vijana niliojuana nao kwa miaka
kadhaa, akiwa na uwezo mzuri wa kujenga hoja, uamuzi na usimamizi, haukuwa
sahihi. Unastahili kukemewa na kukaripiwa.
Uvamizi kama uliofanywa na Makonda utakuwa na madhara zaidi ikiwa
utaachwa na kuenea kwa viongozi wengine wa Serikali hususani wakuu wa mikoa na
wilaya, ama makamanda wa polisi na wengine wenye mamlaka za kuyaamuru majeshi
ya ulinzi na usalama.
Clouds ni chombo huru cha habari, kilichoanzishwa kwa kufuata sheria
za nchi, kikitimiza wajibu wake wa kuuhabarisha umma. Kinapotimiza wajibu wake
kinyume cha sheria, zipo hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Lakini katika kutimiza wajibu huo, Clouds na vyombo vingine vya
habari vinaongozwa na maadili na miiko inayotoa haki sawa ya kusikilizwa kwa
pande zote zinazohusika kwenye habari yenye kulaumiwa kwa upande mmoja.
Na inapotokea hali hiyo, mtoa taarifa hana mamlaka ya kulazimisha
kwa namna yoyote, akiuelekeza utawala wa chumba cha habari kuitumia taarifa
inayolenga ‘kumchafua’ mtu ama iliyo kinyume cha misingi, maadili na miiko ya
uandishi ama utangazaji wa habari.
Inapodaiwa kwamba Makonda aliivamia Clouds ili kushinikiza, kisha
kuchukua sehemu ya taarifa aliyotarajia kuiona ikirushwa katika mazingira
yanayohusisha ushiriki wake katika kuiandaa, ili ‘imchafue’ kiongozi mmoja wa
dini, haipendezi. Umma unapaswa kusema ‘hapana’.
Kwa maana kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa ikiongozwa kwa kuzingatia
sheria, utawala bora na haki za binadamu. Moja ya misingi ya haki hizo ni uhuru
wa habari na uhuru wa kujieleza.
Makonda anapodaiwa kutaka kushinikiza kutangazwa kwa taarifa isiyokidhi
mahitaji ya kimaadili katika tasnia ya habari, inaibua utamaduni wa mamlaka za
utawala kutoheshimu asasi za kitaaluma zinazochangia kwa kiasi kikubwa kasi ya
maendeleo na ustawi wa watu.
Mambo haya yanapojadiliwa haitoi maana ya kumchukia Makonda, la
hasha. Bali kutoridhishwa na mwenendo wa vitendo vyake vinavyoibua uchungu na
mkanganyiko kwa watu wakiwamo wanaomuamini kuwa ni mmoja wa viongozi vijana
wenye uwezo wa kuongoza, lakini wakashindwa kuitumia vizuri fursa hiyo.
0 comments:
Post a Comment