Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
SERIKALI imeitaka kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya
dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu kujenga mtambo nchini kwa ajili ya uchenjuaji
dhahabu.
Nia ni kupunguza malalamiko ya wananchi kuwa madini hayo
yamekuwa yakiibwa kupitia mchanga unaosafirishwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa rai hiyo jana
alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye mgodi wa dhahabu wa Buzwagi iliyodumu
saa moja na kujionea shughuli za uzalishaji kwenye mgodi huo mjini
Kahama.
Alisema Watanzania hawaamini kama mchanga huo una madini
ya dhahabu na shaba.
“Tunataka mjenge mtambo wa uchenjuaji madini ya dhahabu nchini
ili kujiridhisha na mapato yatakayotokana na shughuli mnazofanya kupitia kodi
stahiki ambayo mtakuwa mkilipa serikalini kwa mujibu wa sheria,” alisema
Majaliwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali itakaa na wawekezaji hao
kuona mchakato wa jinsi ya Acacia watakavyojenga mtambo huo na kuondoa lawama za
Watanzania kuwa madini hayo yamekuwa yakiibwa.
Aidha, Majaliwa alisema wazekezaji hao kama watajenga
mtambo huo nchini, Serikali itapata mapato makubwa zaidi hali
ambayo itasaidia ukuzaji wa uchumi kutokana na kodi stahiki ambayo italipwa nao.
Waziri Mkuu alisema moja ya makubaliano ya wawekezaji hao
na Serikali tangu mwaka 2009 ni kujenga kiwanda cha uchenjuaji madini nchini.
Alisema wawekezaji hao wakijenga mtambo huo nchini pia wataongeza
ajira kwa Watanzania wengi huku akiisisitiza kampuni hiyo kutopunguza
wafanyakazi kutokana na Serikali kuzuia usafirishaji wa kontena zao za mchanga
wa dhahabu kwenda nje.
“Kwa sasa nimekuja kuangalia uzalishaji wa dhahabu na
kontena zilizo kwenye mgodi wenu na kuchukua sampuli ya mchanga unaosadikiwa
kuwa asilimia 50 yake ni madini ya dhahabu na asilimia 50 nyingine ni madini
mengine ambayo ni shaba,” alisema Waziri Mkuu.
0 comments:
Post a Comment