Mwandishi Wetu
Dk. Juma Malewa |
WAKUU wa Shirika la Uzalishajimali la Jeshi la Magereza nchini wametakiwa
kuongeza jitihada za uzalishaji.
Pia limetakiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kila miezi
mitatu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ununuzi wa Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi, David Mwangosi, wakati akizungumza na makamanda wa shirika
hilo jana Dar es Salaam.
Mwangosi alisema shirika hilo linapaswa kuwa chachu ya uzalishaji wa
mazao ili kutosheleza wafungwa na jamii zingine.
Alisema iwapo kila kiongozi atasimamia majukumu yake na kuongeza
uwajibikaji, ni dhahiri uzalishaji utaongezeka hivyo kutimiza matarajio ya
Serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Mkurugenzi alisema viongozi wanaosimamia shirika hilo wanapaswa
kuwa wabunifu kwa kushawishi wadau ili kushirikiana katika miradi mbalimbali.
“Nimekuja hapa kumwakilisha Katibu Mkuu, Meja Jenerali mstaafu Projestus
Rwegasira ambaye amesema hataki mzaha katika kazi na anataka kila miezi mitatu
muwe mnamletea taarifa ya shirika,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi huyo aliwataka makamanda wanaosimamia shirika na
miradi kuhakikisha wanaanzisha viwanda vidogo kwani ni chachu ya maendeleo.
Mwangosi alisema wizara iko tayari kuunganisha Magereza Tanzania
na nchi mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia uanzishaji wa viwanda hivyo.
Alisema wizara iko tayari kutoa mafunzo ikihitajika hasa kwa wafungwa
ambao watatumiwa katika viwanda husika.
Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Dk Juma Malewa alisema Jeshi
hilo lina miradi takribani 23 ya uzalishaji hivyo linajipanga iwe na tija.
Alisema shirika hilo linajihusisha na uzalishaji wa mahindi,
maharage, mpunga, alizeti, maziwa na nyama na kutokana na changamoto yapo
maeneo ambayo hayajafanya vizuri.
Dk Malewa alisema kutokana na uhaba wa fedha na kuchelewa kwa ruzuku,
uzalishaji wa mbegu bora za kilimo umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka.
Kamishna Malewa alisema shirika linaendelea kutoa chakula kwa wafungwa
na hadi Januari lilishagharimia Sh bilioni 3.6 huku deni kwa taasisi za
Serikali likifikia zaidi ya Sh bilioni 3.
Alisema kwa sasa wanashirikiana na mifuko ya hifadhi za jamii ya NSSF
na PPF kuendeleza shamba la miwa na kiwanda cha sukari chaGereza la Mbigiri na
wanatarajia kuendeleza shamba la mbegu la Bagamoyo lililo na ekari 200.
0 comments:
Post a Comment