Ibrahim Yassin, Mbozi
SERIKALI
wilayani hapa, imewataka wananchi kuachana na vitendo vya ukatili kwa kufanya
mauaji yanayoipa sifa mbaya wilaya hiyo badala ya kufanya kazi za uzalishajimali
kwa kujiunga
kwenye vikundi.
Wilaya hii imekuwa
na sifa mbaya kutokana na matukio ya mauaji
yanayotokana na imani za kishirikina za kupata mafanikio baada ya ramli za
waganga wa kienyeji.
Kauli hiyo
ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John
Palingo, alipozungumza na wanakijiji cha Ipapa kata ya Ipunga alikokwenda
kusikiliza kero zao.
Palingo ambaye
ni Mkuu wa Wilaya, alisema vitendo vya ukatili na mauaji vimekithiri wilayani
hapa hali iliyofanya mkoa wa Songwe kushika nafasi ya pili kwa ukiukaji wa haki
za binadamu ikiwa ni pamoja na kupoteza nguvukazi ya Taifa.
Alisema baadhi
ya watu wamekuwa wakienda kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli chonganishi,
huku wakiambiwa wakafanye mauaji na kuchukua baadhi ya viungo kwenye miili yao
kwa imani ya kupata utajiri kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa.
Aidha, aliwataka
wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi uhalifu unapotokea ili
wahusika wakamatwe kwani bila hivyo, Jeshi haliwezi kujua wahalifu ni akina
nani.
Akijibu kwa niaba
ya wenzake, Julius Mwampashe, mkazi wa kijiji hicho kupitia mkutano huo,
alisema wako tayari kutoa ushirikiano kwa kamati ya ulinzi uhalifu utakapotokea
kwa masharti ya kutowataja.
Mwampashe
aliongeza kuwa kumekuwa na ugumu kwa baadhi ya wananchi kutoa ushirikiano hasa
kwa Jeshi la Polisi pindi uharifu unapotokea kutokana na kuwataja na kusababisha
maisha yao kuwa hatarini.
0 comments:
Post a Comment