Asha Kigundula
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Klabu ya
Yanga, wameamua kutolala kwa kuendelea na mazoezi ikionesha inataka kutetea
ubingwa wake na kufanya vizuri katika michezo ya Ligi, Kombe la Shirikisho (FA)na
kimataifa dhidi ya MC Alger ya Algeria mwezi ujao.
Katika mbio za kutetea Yanga itacheza mchezo wa kiporo dhidi
ya Azam FC, utakaofanyika Aprili mosi mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam.
Pia itakuwa ikijifua kwa ajili michezo mingine ya ligi na
wa Kombe la Shirikisho dhidi ya MC Alger utakaofanyika Dar es Salaam kati ya
Aprili 7 na 9 kabla ya kurudiana wikiendi inayoangukia Aprili 14 na16, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alisema
wachezaji waliosalia kwenye kikosi baada ya wengine kuitwa katika timu ya taifa
na wengine majeruhi wameanza mazoezi juzi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi
uliopo Kurasini, Dar es Salaam.
Mkwasa alisema licha ya kuanza mazoezi hayo, kambi ya
timu hiyo itaanza wiki ijayo baada ya kumalizika kwa mchezo kimataifa wa
kirafiki wa timu ya Taifa, Taifa Stars dhidi ya Botswana, wachezaji walio
katika timu hiyo wataungana na wenzao.
Kikosi cha Yanga kina wachezaji watano Taifa Stars ambao
ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Vicent Andrew na Simon Msuva.
Hata hivyo alisema washambuliaji Amissi Tambwe na Donald
Ngoma, hawajaungana na wenzao katika mazoezi yanayoendelea kutokana na
umajeruhi. Mkwasa alisema hana taarifa za maendeleo ya wachezaji hao, lakini kuna
taarifa kutoka katika benchi la ufundi kuwa hawatacheza mchezo huo dhidi ya
Azam FC.
“Tambwe na Ngoma bado majeruhi hawatacheza mchezo huo
dhidi ya Azam kwa sababu wanaendelea na matibabu, watakuwa nje kwa muda wa wiki
10 kwa kuwa hawajapata nafuu ya kufanya waweze kuanza mazoezi na kuungana na
wenzao,” kilisema chanzo jana.
Wawili hao, wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu, Tambwe
ameumia goti na Ngoma ameshitua kifundo cha mguu baada ya kuumia kwenye
michuano ya Kombe la Mapinduzi, visiwani Zanzibar.
Yanga inakabiliwa na mchezo huo mgumu wa ligi dhidi ya
Azam FC ambao matokeo yake yatatoa sura ya kuendelea kupigania ubingwa wao walioupata
uliopita, kwa sawa wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa na pointi
53, wakizidiwa na watani wao wa jadi Simba alama mbili.
0 comments:
Post a Comment