Emeresiana Athanas
Dk Elly Macha |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimepata pigo baada ya Mbunge wake wa Viti Maalumu, Dk Elly Macha kufariki
dunia kwa maradhi.
Taarifa ya kifo cha Mbunge hiyo
iliyotolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene jana ilisema Dk Macha
alifariki dunia jana kwenye hospitali ya New Cross Wolverhampton, Uingereza
ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu.
"Kifo cha Mbunge wetu ni pigo
kwetu, kwa Bunge na Taifa kwa ujumla, kwani wakati wa uhai wake alikuwa mchango
mkubwa katika masuala ya kichama na bungeni pia alikuwa makini kupigania
maslahi ya wananchi na hasa kundi la watu wenye ulemavu kwani alikuwa
mwakilishi wao," alisema Makene.
Taarifa ya Spika wa Bunge iliyotolewa
Dar es Salaam jana ilisema mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kurudishwa
nchini inaendelea kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
"Mipango ya kusafirisha mwili kuja
nchini ikiwa na taratibu za mazishi zinafanyiwa kazi. Taarifa zaidi juu ya
msiba huo zitaendelea kutolewa kwa kadri zitakavyopatikana," ilisema
taarifa hiyo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema Dk Macha alikuwa mmoja wa watu waliojitolea utaalamu na taaluma zao
kukitumikia chama chao.
"Msiba huu ni moja ya mapigo makubwa
kwetu sisi Chadema na Watanzania, kwani alitumia uzoefu wake kushauri chama
katika masuala mbalimbali na kuwa mstari wa mbele katika haki kwa watu wenye
ulemavu bungeni.
"Alifanya hivyo akiwa mwanachama wa
kawaida hadi hapo alipogombea nafasi ya mjumbe wa Kamati Kuu na baadaye kuwa
Mbunge wa Viti Maalumu," alisema Mbowe.
Alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa
familia, ndugu, marafiki, viongozi wa chama, wanachama, na wote walioguswa na
msiba huo.
Marehemu alichaguliwa mjumbe wa Kamati Kuu
katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama mwaka 2014 na mwaka juzi alikuwa kati ya
wagombea waliojitokeza kuwania uteuzi wa ubunge wa viti maalumu.
0 comments:
Post a Comment