Suleiman Msuya
Jenerali Venance Mabeyo (katikati) akizungumza |
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance
Mabeyo amesema suala la ulinzi halina mbadala na kwamba kusitisha huduma yoyote
kwa jeshi hilo ikiwemo umeme ni kuhatarisha usalama wa nchi.
Mabeyo ametoa tahadhari hiyo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Upanga Dar es Salaam kuhusu deni wanalodaiwa na Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) ambalo ni zaidi ya Sh. bilioni 3.
Mkuu huyo wa majeshi alikiri kuwa
wanadaiwa fedha hizo na Tanesco na kwamba leo watalipa Sh. bilioni moja ili
kupunguza dani hilo.
“Tanesco itambue kuwa jeshi ni chombo
muhimu kwa Taifa na kwamba kukikatia umeme ni kuhatarisha usalama wa nchi,” alisema
Jenerali Mabeyo na kuongeza:
“Deni hilo linatokana na ufinyu wa
bajeti jambo ambalo tunajipanga kukabiliana nalo.”
Alisema deni hilo linahusu vikosi vyake
mbalimbali vinavyotumika katika uzalishaji, ulinzi na utawala hivyo Tanesco
haina sababu ya kukimbilia kukata umeme kwani shughuli nyingi zitasimama.
“Nawaomba watuvumilie, lakini pia
watambue kuwa kukata umeme katika ni hatari kwa nchi,” alisisitiza.
Alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa
deni hilo linaisha huku akibainisha mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato
katika jeshi hilo kupitia Kikosi cha Nyumbu, Suma JKT na Mzinga.
Ulipaji wa deni hilo unakuja takribani
wiki mbili baada ya Tanesco kutoa wiki mbili zilizoisha jana kuwa litakata
umeme kwenye taasisi za Serikali na sekta binafsi ambazo zimekuwa wadaiwa sugu
ambapo JWTZ ni moja wapo.
Taasisi nyingine ilikuwa ni Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambapo ilikuwa inadaiwa zaidi ya bilioni 121 na
Tanesco na hivi karibuni ilipunguza deni hilo kwa kutoa Sh. bilioni 10.
Mabeyo alisema vikosi hivyo vitaboreshwa
ili kuongeza uzalishaji ikiwa ni kutekeleza lengo la Rais kufikia uchumi wa
viwanda.
Jenerali huyo alisema kwa kuanzia
wameandaa waraka kwa Serikali ili ujadiliwe na Baraza la Mawaziri kuhusu
Shirika Nyumbu kuboreshwa.
Mabeyo alisema lengo lao ni kuhakikisha
kuwa mashirika hayo yanazailisha bidhaa ambazo zinatokana na malighafi za
Kitanzania.
Alisema matumizi katika jeshi hilo
yanaongezeka kutokana na ukubwa wake na mabadiliko ya teknolojia, hivyo ni vema
wakawa na vyanzo vyao vya mapato ili kukidhi mahitaji yao.
“Jeshini kuna mitambo mikubwa ambayo
inalinda nchi lakini pia inazalisha, tekonolijia imekuwa hali ambayo inachangia
ongezeko la matumizi ya umeme hivyo vikosi vyetu vikijipanga kuzalisha
vitasaidia mapato,” alisema.
Aidha, Jenerali Mabeyo alisema jeshi
hilo linadaiwa na wazabuni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma hali ambayo
inasababishwa na ufinyu wa bajeti.
Mkuu huyo wa majeshi alisema jeshi hilo
lipo imara katika kulinda usalama wa nchi na kuwataka wananchi kuendelea kutoa
ushirikiano kwao kwa maslahi ya nchi.
0 comments:
Post a Comment