Suleiman Msuya
CEO QGL, Nicholas Ralph |
KAMPUNI ya Quality Group Limited
(QGL), inaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya
rushwa na ufisadi.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizoko barabara ya Nyerere,
Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL, Nicholas Ralph alisema katika
kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi kampuni imeanzisha mfumo unaotambua na
kudhibiti uhalifu huo kwenye taasisi (e-Governance).
Alisema mfumo huo wa utambuzi na
udhibiti unapaswa kuwepo katika idara zote za Serikali, kwani una tija na ni
salama zaidi hasa katika kuelekea katika Tanzania ya maendeleo endelevu.
Ralph alisema QGL imewekeza katika
sekta mbalimbali kama afya ambapo wanatarajia kujenga vituo 4,000 vya afya
nchini pamoja na vibanda vya kutoa afya ili kuendana na teknolojia ya sasa na
kurahisisha kila mwananchi anapata huduma bora ya afya.
Alisema pia wamekubaliana na kampuni
kutoka Urusi ili kusambaza vifaatiba na kampuni nyingine kutoka Marekani itatoa
huduma ya ndege kwa huduma za dharura.
“Pia kampuni ya QGL imeingia
makubaliano na kampuni ya Ireland kujenga na kusimamia viwanja vya ndege na
kusaidia mafunzo ya teknolojia ya huduma za viwanja hivyo na hifadhi ya mafuta
ya ndege,” alisema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa QGL, alisema
kampuni ya QGL imekuwa ikisadia wavuvi wa Kanda ya Ziwa kwa kuwapa vitendea
kazi na matibabu, kusaidia elimu na pia ilisaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa
Ebola kwa Afrika.
Alisema kampuni hiyo imefanikiwa kuongeza
ajira, mafunzo, kukuza uchumi ili kuhakikisha inaunga mkono mpango wa maendeleo
wa Serikali wa Mwaka 2025.
Ralph alisema kampuni imekuwa ikitoa
mafunzo kwa viongozi na waajiriwa vijana kupitia programu ya Moreh Derech
ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa.
Aidha, alisema katika kuhakikisha
inapanua ushirikiano na taasisi za kimataifa, imesaini makubaliano na kampuni
ya Solanika International Tractors Limited ya India ambayo itakuwa inaingiza
nchini matrekta 1,000 kwa mwaka, hivyo kuongeza ajira 1,200 ifikapo mwakani.
Hali kadhalika alisema wamewekeza
katika viwanda vya sukari na maziwa ambapo wananchi wengi wa kitanzania ndio
watafaidika kwa kuuza bidhaa husika katika viwanda hivyo venye teknolojia ya
kisasa na uongozi kutoka Israel, Ulaya na Afrika Kusini.
Ralph alisema QGL imekuwepo kwa zaidi
ya miaka 30 ambapo inashirikiana na kampuni kubwa duniani kama General Motors
(GM), Honda, Isuzu, Bridgestone na Chevrolet.
Alisema kutokana na ushirikiano huo,
QGL imeajiri zaidi ya wafanyakazi 667,300 na kupata faida ya dola za Marekani
bilioni 348.6 hayo yakichangiwa na uwajibikaji, uwazi na uaminifu.
Alisema mikakati yao ni kuhakikisha
wanakuwa sehemu sahihi ya kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment