Mwandishi Wetu
Dk Harrison Mwakyembe |
SASA ni dhahiri kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe,
anakabiliwa na wakati mgumu wa utekelezaji wa majukumu yake, kutokana na
mazingira ya kisiasa yanayomzonga.
Jana katika mfululizo wa majanga ya kisiasa yanayomwandama, Dk
Mwakyembe anayejulikana kwa umahiri kwenye sheria nchini, alijikuta katika wakati
mgumu pale agizo alilotoa juzi kwa Watanzania, lilipofutwa na Rais John
Magufuli.
Kabla ya hatua hiyo ya Rais dhidi ya agizo la mteule wake, Dk
Mwakyembe alikuwa katika wakati mgumu wa kisiasa, kutokana na tamko lake
lingine la kutishia kufuta usajili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),
kupingwa na wanataaluma wenzake.
Juzi Dk Mwakyembe aliagiza kuwa kuanzia Mei mosi viongozi wa Serikali,
mila na dini wanaofungisha ndoa wahakikishe kabla ya kufanya hivyo waoanaji wawe
na vyeti vya kuzaliwa.
Kupingwa kwa tishio hilo na wanasheria, kulienda sambamba na
uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kuwa miongoni mwa wagombea
wa urais wa TLS, jambo lililoonekana kutotiliwa maanani kwa nguvu na ushawishi wa
Waziri huyo kwa wanasheria wenzake.
Itakumbukwa pia kuwa Waziri huyo katika sakata la vita dhidi ya
dawa za kulevya, alijikuta matatani, pale Rais Magufuli aliposema huenda
alidanganywa kuhusu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka
2015, wakati Dk Mwakyembe ni mmoja kati ya washauri wakuu wa Rais katika masuala
ya sheria.
Lakini hata uteuzi uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu wa gwiji
mwenzake wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa Mbunge wa Kuteuliwa na
Rais, kuliibuka minong’ono ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, huku umahiri wa
sheria wa Profesa Kabudi, ukihusishwa na mabadiliko katika Wizara ya Katiba na
Sheria.
Kufutwa agizo
Jana Rais Magufuli alifuta agizo la Dk Mwakyembe siku moja tu
baada ya kutolewa la kuwataka Watanzania wote watakaofunga ndoa kuanzia Mei
mosi, kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Rais amefuta agizo hilo alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi kabla ya kuondoka Ikulu ya
Chamwino, Dodoma kurejea Dar es Salaam.
“Dk Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu masharti hayo
kutumika, kwa kuwa yatawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao
hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa
na changamoto nyingi kwa wanaohitaji,” ilieleza taarifa hiyo ya Msigwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mpaka sasa idadi ya Watanzania walio
na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20, huku wengi wao wakiwa ni waishio
vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa
kabla ya kuanza kutolewa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania, msiwe na wasiwasi wowote,
endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu
chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe
ama aolewe, nitamwelekeza Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe apelike
bungeni kikarekebishwe,” alikaririwa Rais Magufuli na taarifa hiyo.
Aidha, Rais Magufuli alitoa mwito kwa Watanzania kuendelea kupata
vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na kutaka viongozi wote kuhamasisha
wananchi kuwa na vyeti hivyo.
Tishio la TLS
Rais Magufuli alifuta agizo la Mwakyembe, wakati Waziri huyo
akijadiliwa katika majukwaa ya kisheria na kisiasa, kutokana na kauli yake ya
kutishia kufuta Sheria ya TLS Sura ya 307 iliyoanzisha chama hicho.
Dk Mwakyembe akizungumza na ugeni wa TLS uliomtembelea ofisini
kwake Dodoma ukiongozwa na Rais wao, John Seka, alikaririwa akisema kuwaingiza
wanachama wenye nasaba za siasa au viongozi wa vyama vya siasa ndani ya TLS, ni
kuruhusu mgongano wa maslahi na yeye ni mwanasheria hivyo hawezi kukubali jambo
hilo.
“Wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS ikijiingiza
katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya kuitawala TLS, ila
tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa sheria yenu iko chini yetu.
“Mkiharibu kwa lolote, Wizara ndiyo yenye wajibu wa kuwatolea maelezo
na katika hilo mnalotaka kulifanya sasa, kuna mgongano wa maslahi, je ninyi
kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?” Alihoji Mwakyembe.
Mbali na wanasheria kadhaa kumpinga kwa kauli hiyo, Chama cha
Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kilimwandikia barua ya wazi Mwakyembe,
iliyosainiwa na Rais wake, Richard Mugisa kumtaka aache kuingilia uchaguzi wa
TLS.
Barua hiyo iliungwa mkono na TLS, pale Seka alipoeleza
kufurahishwa kwake na barua hiyo na kufafanua kuwa chama hicho kilikuwa mbioni
kukutana na Mwakyembe ili kujadili mustakabali wa chama hicho.
Mgombea TLS
Kama haitoshi, Lissu na kada mwingine wa Chadema, aliyewahi kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha walithibitishwa kuwa wagombea urais wa
chama hicho, kinyume na maoni ya Dk Mwakyembe na Rais Magufuli kuhusu wanasiasa
na chama hicho.
Wengine walioidhinishwa kugombea nafasi hiyo ni pamoja na
aliyewahi kuwa Rais wa TLS, Francis Stola, aliyewahi kuwa mgombea urais kupitia
CCM mwaka 2015, Godwin Mwapongo na Wakili Victoria Mandari.
Mbali na kuthibitishwa kuwa wagombea katika uchaguzi unaofanyika
leo, lakini hata kesi mbili zilizofunguliwa Mahakama Kuu Dodoma na Dar es
Salaam kupinga uchaguzi huo, zilitupwa zote juzi.
Kesi ya Dodoma ilifunguliwa na Wakili Godfrey Wasonga, akipinga
uchaguzi huo akidai kuwa kanuni za uchaguzi huo ni batili; huku ya Dar es
Salaam ikifunguliwa na Wakili Onesmo Mpinzile, dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, nayo dhidi ya kanuni hizo za uchaguzi.
Kufichwa sheria
Mwakyembe alijikuta katika wakati mgumu katika sakata hilo la TLS,
siku chache baada ya Rais Magufuli kutamka wazi kuhusu uwepo wa njama za kumficha
Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam Februari 12, Rais Magufuli alisema
Waziri Mkuu na mawaziri walifichwa sheria hiyo na hata Waziri Mkuu alifichwa
kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Kupambana na Dawa za Kulevya.
“Waziri Mkuu mwenyewe alijua jana au juzi kwamba ndiye Mwenyekiti
wa Baraza hilo,” alibainisha Rais Magufuli. Alisema hana uhakika kama mawaziri
husika kwenye Baraza hilo walikuwa na taarifa ya kuwa wajumbe, maana walifichwa
na wasaidizi wao wizarani, hadi walipoelezwa na Waziri Mkuu kwamba wanawajibika
kupambana na dawa za kulevya.
Rais Magufuli alisema kutokana na ugumu uliopo hata ndani ya
Serikali, ndiyo maana hakuwahi kupelekewa jina ili ateue Kamishna wa Mamlaka ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, hadi alipoamua mwenyewe kumteua kwa
njia alizozijua.
“Nilikuwa najiuliza kwa nini sijaletewa mapendekezo ya uteuzi wa
Kamishna wa Dawa za Kulevya, baada ya kuona kimya nikaamua kuteua mwenyewe, kwa
hiyo mnaona vita hivi vilivyokuwa vikubwa, ndani ya Serikali si malaika,”
alikaririwa Rais.
Kabudi
Januari Rais Magufuli aliteua wabunge wawili, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo na nguli wa sheria, Profesa Kabudi,
ambaye alihusishwa moja kwa moja na uwezekano wa mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri.
Katika mtazamo huo, Profesa Kabudi kwa weledi wake alihusishwa na
mabadiliko katika Wizara ya Katiba na Sheria, inayoongozwa na Dk Mwakyembe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana
alikaririwa akisema: “Siwezi kuwa mtabiri, lakini ukisoma alama za nyakati na
uteuzi huu kufanyika sasa, inawezekana si wote, lakini nafikiri anaweza (Rais
Magufuli) kufanya mabadiliko katika Baraza lake.
“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi na anaijua Tanzania. Ana
uwezo mkubwa wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani kama Rais atamwacha hivi hivi
akiwa mbunge tu.”
0 comments:
Post a Comment