TCCL yapewa miezi miwili kupata Sh. bilioni 100


Mwandishi Wetu

Profesa Makame Mbarawa
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  Profesa Makame Mbarawa, ameipa miezi miwili  Kampuni ya Simu Tanzania  (TTCL), kuhakikisha inapata dola za Marekani milioni 50 (Sh.bilioni 107.5) ili kuongeza pato kwa kampuni na Taifa.

Mbarawa ametoa agizo hilo mjini Bukokba jana ambapo alisema limetokana na Serikali kuongeza masafa kwa kampuni hiyo kutoka 10 hadi 200 (MHZ) ambayo yana uwezo wa kuunganisha wateja wengi na wakubwa zaidi.

"Hakikisheni mnajipanga kuipata hiyo fedha ndani ya miezi miwili na kuwapatia masafa ya kutosha wateja mlionao ndani na nje ya nchi na kujitahidi kuongeza wateja wengi zaidi", alisema Prof. Mbarawa.

Alisisitiza kampuni za simu nchini kuchangamkia fursa ili kupata masafa yenye uwezo mkubwa kupitia Mkongo wa Taifa.

Aidha, ameitaka TTCL kuongeza  wigo wa kuwasiliana na wateja wakubwa ili kuwashawishi kununua masafa hayo  kulingana na mahitaji yao, hivyo kuongeza wigo wa kibiashara  na kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa TTCL Mkoa wa Kagera,  Salum Mbaya aliihakikishia Serikali kuwa wataanza mara moja kazi ya kutembelea wateja wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwapatia taarifa za ongezeko la uwezo wa mkongo na kuwashiwishi kujiunga ili kupatiwa masafa wanayohitaji.

Mbaya ametaja kuwa mpaka kufikia sasa nchi zilizounganishwa na mkongo wa Taifa  ni Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Kenya na Malawi.

Aidha, Waziri Mbarawa alitembelea Uwanja wa Ndege wa Bukoba na kuahidi kutatua changamoto zinazoukabili uwanja huo ikiwemo kujenga jengo la kuongozea ndege ili kuongeza ufanisi na usalama katika usafiri wa anga.

Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini mkoa wa Kagera,  Dorice Uhagile, licha ya kuelezea mafanikio mbalimbali kama vile ongezeko la ndege na wateja uwanjani hapo pia amefafanua changamoto mbalimbali zinazoukabili uwanja huo na kuiomba serikali iweze kuwatatulia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo