*Kumshitaki Sekretarieti ya Maadili na Tume
Mwandishi Wetu
Meya wa Manispaa ya Boniface Jacob |
MEYA wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, amesema yuko katika hatua
za mwisho kufungua kesi mahakamani dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kwa madai ya kughushi vyeti vya elimu na nyaraka zingine.
Kwa mujibu wa Jacob, kesi hiyo itajikita kwenye maeneo manne makuu
ambayo ni; Mkuu huyo kujifanya Paul Makonda, kula kiapo kwa Rais kwa niaba ya
Paul Makonda, kujitambulisha ukuu wa mkoa na kutumia nyaraka kwa jina la Paul
Makonda ambazo si za jina lake wakati yeye ni Daud Albert Bashite.
Jacob alisema hayo alipozungumza na gazeti hili jana akibainisha
kuwa pamoja na kufungua kesi hiyo, pia atamshitaki Makonda kwenye Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).
Meya alisema wakili wa kesi hiyo atakuwa Peter Kibatala na
wanasheria wengine wengi aliosema wamejitolea kusaidia ili ukweli ujulikane.
Alisema hafanyi hilo kwa nia ya kumkomoa Makonda, bali kutaka kuhakikisha haki
inatendeka kama ilivyotokea kwa watu wengine.
“Kuanzia Jumatatu, natarajia kufungua kesi mahakamani ambayo
itamhusu Makonda kwa tuhuma za kughushi vyeti na kufanya kazi kwa jina lisilo
lake,” alisema. Alisema atafuata taratibu zote muhimu kabla ya kufungua kesi
hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Alisema kitendo cha mtu kutengeneza nyaraka kwa jina ambalo lisilo
lake ni kosa la jinai ambao haliwezi kuvumiliwa. Aidha, alisema Sekretarieti na
Tume, anaamini kuwa ni vyombo vyenye mamlaka kwa watumishi wa umma.
Sakata la Makonda kudaiwa kughushi vyeti liliibuka katika mitandao
ya kijamii takriban mwezi mmoja uliopita na kila alipoulizwa amekuwa akishindwa
kulizungumzia hata wakati mwingine kutoa lugha chafu kwa waandishi wa habari.
Baadhi ya waandishi ambao walikumbwa na lugha chafu za Mkuu huyo
wa Mkoa ni Mhariri wa Habari wa Gazeti hili, Exuperius Kachenje na mwandishi wa
Tanzania Daima, Ibrahim Yamola.
Gazeti la JAMBO LEO lilikuwa la kwanza kuandika habari kuhusu elimu
ya Makonda baada ya taarifa za mtandaoni kabla ya vyombo vingine vya habari
hasa magazeti na mitandao ya kijamii, kuendelea kufuatilia huku Askofu wa
Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat Gwajima akijitokeza na kudai kuwa na ushahidi
wa kutosha kuhusu kiongozi huyo kughushi vyeti.
Wamshangaa
Akizungumzia kitendo cha Makonda kusafiri nje ya nchi safari zisizo
na tija, licha ya katazo la Rais John Magufuli, mkazi wa Dar es Salaam, Joel
Nkwale alisema ni jambo la kushangaza kwa kiongozi huyo kusafiri wakati Rais
yuko nchini.
“Kama sijakosea mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyapinga ni
matumizi mabaya ya fedha za umma na Makonda amesafiri Marekani, Ufaransa na
Afrika Kusini, sijui anatumia fedha za nani mbona hili halisemwi?” Alihoji
Nkwale.
Joyce Temba wa Mwananyamala, alihoji Mkuu wa Mkoa alikopata fedha
za kufanyia sherehe za mwaka mmoja na kurusha matangazo ya mbashara kwa zaidi
ya saa tatu kwenye vituo tofauti vya televisheni, licha ya Rais kukataza matangazo
mbashara kwa Bunge.
0 comments:
Post a Comment