Celina Mathew
Haelemariam Dessalegn |
WAZIRI Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Ethiopia, Haelemariam Dessalegn, anatua nchini leo kwa ziara ya
siku mbili ambapo pamoja na kusaini mikataba mitatu atatembelea Mamlaka ya Usimamizi
wa Bandari Tanzania (TPA).
Mikataba hiyo itahusu maeneo ya biashara
na uwekezaji hususan kwenye utalii, viwanda na nishati ya mafuta huku mingine
ikiwa ya kidiplomasia.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, Dk Suzan
Kolimba alisema ujio huo ni mwaliko wa Rais John Magufuli.
Aliswema Rais alimwalika Dessalegn
kwenye mkutano wa pembezoni mwa mkutano wa kawaida wa 28 wa wakuu wa nchi na
serikali wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia mwaka huu.
"Dessalegn anatarajiwa kuwasili asubuhi
na atapokewa na Rais Magufuli na madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano mzuri
kati ya nchi hizo pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo
mbalimbali ukiwamo uwekezaji na biashara," alisema.
Alisema wakati wa ziara hiyo, atafanya mazungumzo
na Rais Magufuli na wajumbe wa pande mbili ambapo viongozi hao watashuhudia
uwekaji saini mikataba ya ushirikiano kabla ya kuzungumza na waandishi wa
habari.
Dk Kolimba alisema kesho ataendelea na
ziara yake bandarini kujionea shughuli zinazofanyika na kisha wataondoka kurudi
kwao.
Akizungumzia uhusiano kati ya nchi hizo
mbili, Dk Kolimba alisema ni mzuri na nchi hiyo imeonesha nia ya kufungua
ubalozi nchini hivi karibuni kwani sasa inawakilishwa
na balozi wake aliye Kenya.
0 comments:
Post a Comment