Dotto Mwaibale
WAFANYABIASHARA wanawake kwenye masoko
jijini Dar es Salaam wamejitambua na kujitokeza kugombea uongozi katika maeneo
yao ya biashara.
Hayo yamebainishwa na Mwezeshaji wa
Kisheria katika Soko la Tabata Muslim, Irene Daniel wakati akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu faida waliyopata kutokana na mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia sokoni
kupitia Shirika la Equality for Growth (EfG)
"Kwa kweli wanawake hivi sasa tuko
imara, tunajitambua na tuna uthubutu baada ya kupata dozi kutoka EfG kwani hapo
awali tulikuwa waoga na hatukujua haki zetu ndiyo maana tulikuwa nyuma
kimaendeleo," alisema Irene.
Alisema baada ya mafunzo hayo na
kuwezeshwa kujua sheria na mambo yaliyokuwa yakimdhalilisha mwanamke, hali ni
shwari katika masoko kwani hivi sasa wanafanya biashara zao katika mazingira
salama.
Alisema kutokana na hali hiyo wanawake
wamejitokeza kugombea uongozi na kuwa wajumbe katika kamati za masoko jambo
ambalo ni la kujivunia.
Mfanyabiashara mwingine kwenye soko hilo
ambaye pia ni Mwezeshaji wa Kisheria, Aisha Juma alisema taaluma waliyopata
kupitia EfG imesaidia kuweka mambo sawa na ushirikiano baina yao kwenye masoko
kwani leo hii hakuna mtu wa kumnyanyasa mwenzake kutokana na jinsia yake na
anayebainika amekuwa akichukuliwa hatua.
0 comments:
Post a Comment