Nape Nnauye |
ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ameahidi kumwunga mkono Waziri mpya Dk Harrison
Mwakyembe na kuendeleza uaminifu wake kwa Rais John Magufuli.
Nape alitoa kauli hiyo jana Dodoma wakati akikabidhi ofisi kwa Dk Mwakyembe ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa Serikali
yanapotokea mabadiliko.
“Tofauti na maneno ya mitandaoni, nitabaki kuwa
mtiifu kwa Rais, Serikali na CCM,” alisema Nape.
Nape aliondolewa kwenye wadhifa huo wiki iliyopita
baada ya kuongoza wizara hiyo kwa takriban miezi 15, alimshukuru Rais Magufuli
kwa kumwamini na kumpa dhamana kubwa ya kusimamia wizara kwa kipindi hicho,
huku akiwa mbunge kwa mara ya kwanza.
Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na wizara kwa
ukaribu akikiri kuwa yeye ni mdau mkubwa wa sekta za wizara hiyo.
“Heshima aliyonipa Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumwunga mkono katika
dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini,” alisema.
Alishukuru watendaji wote wa wizara kwa kumpa ushirikiano
wa kutosha kwa kipindi chote alichofanya nao kazi na kuwaomba kutoa ushirikiano
huo huo kwa Dk Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe aliahidi kushirikiana na Nape kwa kuwa ni mdau mkubwa
katika sekta hiyo.
Aidha, Mwakyembe aliahidi kuendeleza
mazuri yaliyoanzishwa na Nape katika kuimarisha ufanisi wa wizara hiyo na
kuhakikisha inakuwa moja ya wizara za mifano nchini.
Alisema Nape amefanya kazi kubwa ya
kuitangaza wizara hiyo hivyo matarajio yake ni kuona jitihada hizo
zinaendelezwa kwa kasi zaidi.
“Naahidi kushirikiana na aliyekuwa
waziri, kwani mchango wake ni mkubwa sana hivyo yale mazuri lazima twende nayo
kwa kasi ile ile,” alisema.
0 comments:
Post a Comment