Kamati: Makonda alitumia ‘unga’ kuwatisha Clouds


*Ni baada ya kukataa kurusha kipindi chake
*Yapendekezwa Mamlaka imchukulie hatua

Celina Mathew na Abraham Ntambara

Nape Nnauye
KAMATI ya Waziri Nape Nnauye ya kuchunguza uvamizi wa kituo cha Clouds Media, imebaini kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitumia tuhuma za dawa za kulevya kutisha wafanyakazi wa kituo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume hiyo kwa Waziri Nape jana, iliyosomwa na mjumbe Deodatus Balile, usiku wa uvamizi wake Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliwalazimisha wafanyakazi hao kurusha kipindi chake, vinginevyo angewaingiza kwenye tuhuma hizo.

“Baada ya hapo aliwatisha kuwa yote yaliyotokea usiku ule yabaki pale pale ndani … palikuwa na vitisho kwa walinzi na wafanyakazi kwa kutumia askari wenye silaha,” ilisema taarifa.

Aidha, ilibainisha kwamba Mkuu wa Mkoa aliwatishia watangazaji wa kituo hicho kuwaweka ndani kwa miezi sita bila kufikishwa mahakamani, iwapo wangetoa taarifa hizo nje na kuwaunganisha wadhamini wa kipindi hicho kwenye tukio tuhuma za mihadarati.

Kubainika kwa tabia hiyo kwa Makonda kunaweza kuhusishwa na hatua yake ya kutaja hadharani majina ya watu aliodai wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya mapema Februari.

“Makonda aliwatishia watangazaji wa Clouds kuwa endapo wangetoa taarifa hizo nje angewafunga kifungo cha miezi sita jela au kuwahusisha na tuhuma za dawa za kulevya, pia wadhamini wa kipindi wangeunganishwa kwenye tukio hilo,” alisema Balile.

Alisema kabla ya kumhoji Mkuu wa Mkoa, Machi 20 walifanya mahojiano na wafanyakazi wa Clouds na kujumuisha waliokuwa kazini pamoja na viongozi wao.

Alieleza kuwa pia walifanyia uchunguzi picha za kamera za CCTV ambazo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, uchunguzi uliofanywa kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 4 usiku.

Alisema Machi 21 saa 5.10 walifika ofisini kwa Makonda ambako waliambiwa yuko ofisini na ilipofika saa 6.30 walipoambiwa wamfuate ofisini, na wakati wakipanda ngazi, kiongozi huyo aliwakimbia kwa kupitia mlango wa nyuma.

Matokeo

Balile alisema baada ya Kamati kuchunguza kwa kina ilibaini kuwa siku ya tukio, Machi saa 4.30 usiku, Makonda alifika ofisi za Clouds akiendesha gari namba T553 DFH akifuatana na askari wenye silaha za moto.

Alisema lengo lilikuwa ni kushinikiza kurushwa kwa kipande cha video katika kipindi cha De Weekend Chat Show ‘Shilawadu’ ambacho kilikuwa na kashfa dhidi Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Maoni

Alisema Kamati ilibaini kuwa kitendo alichofanya Mkuu wa Mkoa kina viashiria vya uvunjifu wa sheria za nchi hususan za utangazaji na huduma za habari.

Aidha, alisema pia ilibaini kuwa Mkuu wa Mkoa hatambui madaraka makubwa aliyonayo na kujikuta akiyatumia vibaya katika mazingira yasiyostahili.

Pia alisema walibaini kuwa uongozi wa Clouds unastahili pongezi kwa kusimamia misingi, sheria na maadili ya uandishi wa habari kwa kukataa kurusha habari isiyo na mizania.

Mapendekezo

Kuhusu mapendekezo Kamati ilitaka Makonda aombe radhi wafanyakazi wa Clouds Media Group na vyombo vya habari kwa ukiukwaji wa usalama na maadili ya vyombo vya habari.

Pia katika kulinda maslahi ya tasnia ya habari, Kamati ilimtaka Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye ndiye mwenye dhamana, kuwasilisha malalamiko rasmi ya wanahabari dhidi ya Makonda kwa mamlaka ya uteuzi ili imchukulie hatua stahiki.

Kadhalika vyombo vya Dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia na silaha kwenye kituo hicho, ili kudhibiti matukio ya aina hiyo yasijirudie siku za usoni.

Aidha, Kamati iliitaka Clouds Media ipitie upya miongozo, kanuni, sheria na taratibu zinazoongoza shughuli za utangazaji na kuangalia njia bora za udhibiti wa watu wanaoingia ovyo ndani ya ofisi zake na kujipa majukumu yasiyowahusu.

Nape

Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Nape aliahidi kuiwasilisha kwa viongozi wake wa juu ambao ni Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambao ndio watatoa uamuzi.

Alikiri kuwa kazi haikuwa ndogo, kwa kuwa ilihusisha tukio la kihistoria ambalo halijawahi kutokea nchini huku akiwataka wananchi kuwa na tabia ya uvumilivu wakati uchunguzi ukifanyika.

“Wakati uchunguzi unafanyika, kuna watu walikuwa wakipiga simu sana na wengine wakizungumza maneno hivyo nawaomba Watanzania tujenge utaratibu wa kuvumiliana na kuaminiana, tukiri kwamba sisi ni binadamu kunaweza kuwepo udhaifu, hivyo unapojitokeza inabidi tuvuliane, maana udhaifu si tope kwa viongozi wote,” alishauri.

Tume yalaani

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelaani kitendo cha Makonda kuvamia ofisi za Clouds Media Group.

Aidha, imesema kitendo hicho kinapingana na ibara ya 18 ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977 inayolinda uhuru wa maoni na mawasiliano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga ni jambo ambalo pia linalindwa na ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966 na ibara ya 9 ya mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu ya mwaka 1986.

“Tume imepitia sheria kadhaa ikiwamo ya tawala za mikoa sura ya 97 ya sheria za Tanzania na imebaini kwamba hakuna sheria inayomruhusu Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za uvamizi kama alivyofanya Makonda,” alisema Nyanduga.

Alisema hatua ya kuvamia kituo hicho akiambatana na askari wenye silaha ni kitendo kisichojali wala kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu.

Nyanduga alisema ni kitendo cha kujichukulia sheria mkononi na kisichokubalika katika jamii au nchi ya kidemokrasia.

Ili kulaani kitendo hicho, Tume ilishauri Makonda akiri kuwa kitendo hicho ni uvunjifu wa haki za msingi za waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa kitendo cha kuvamia ofisi hiyo kwa kutumia askari wa Polisi kwa maslahi binafsi hakiendani na utawala wa sheria na hivyo Makonda amelidhalilisha Jeshi hilo na hivyo si budi awaombe radhi Watanzania.

Malalamiko

Wakati huo huo, Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob amewasilisha malalamiko matano kwa Tume ya Maadili inayosimamia uwajibikaji kwa viongozi wa umma dhidi ya Makonda.

Akiwasilisha malalamiko hayo kama mwananchi wa kawaida jana, alisema hatua hiyo inakuja baada ya kupokea maoni ya wabunge zaidi ya 40 ambao wengi wao ni wa CCM waliompigia simu kumwomba aondoe shauri hilo mahakamani na badala yake apeleke kwa Tume hiyo ili waweze kumjadili bungeni.

“Wabunge wengi walionipigia ni wa CCM, wakisema wana hamu ya kumchambua Makonda, hivyo kwa kuwa Tume haina haki ya kumwondoa mtu kwenye uongozi hapana budi kusubiri majibu yake,” alisema.

Alitaja malalamiko hayo kuwa ni pamoja na vyeti vyake ambapo wakihitajika walimu na wanafunzi wataletwa, matumizi mabaya ya madaraka, namna ambavyo anatumia watuhumiwa kujipatia mali, ukiukwaji wa matumizi mabaya ya ofisi za umma kwa kudhalilisha watu kwa kuwataja majina na kupokea zawadi bila kutangaza.

“Tunaamini kwamba Tume itasaidia, maana umma unalalamika lakini viongozi wa juu wanamwogopa Makonda wakati ni mtumishi wa kawaida, Waziri Mkuu amekosa uthubutu hivyo tunataka kujua kama Jaji Mkuu naye anamwogopa,” alisema.

Jacob aliongeza kuwa inawezekana Rais John Magufuli alitaka vitu ambavyo havizungumzwi kwenye mitandao na badala yake waende kulalamika kwenye Tume husika, jambo ambalo amelifanya.

Alifafanua kuwa alichofanya ni namna Rais alivyomwagiza na kueleza mwavuli aliotumia Makonda wa kusema anapambana na dawa za kulevya, si kweli maana vita hivyo vilianza muda mrefu na anavitumia kuficha maovu yake.

Jacob alimkabidhi Msaidizi wa Kamishna wa Maadili, Dora Mgeta nakala za picha nne na kadi za magari na ambaye alimwahidi Jacob kuwa malalamiko hayo yatajibiwa
kwa barua.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo