Charles James
Dk John Magufuli |
WAMILIKI wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuwa makini na
habari zinazochapishwa kwenye vyombo vyao na wasidhani kuwa uhuru walionao
hauna mipaka.
Onyo hili lilitolewa jana na Rais John Magufuli wakati akiapisha mawaziri
wawili aliowateua juzi Alhamisi; Dk Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa kuwa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Profesa Palamagamba Kabudi
aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
Uteuzi wa mawaziri hao ulifanywa na Rais katika mabadiliko madogo kwenye
Baraza la Mawaziri ambapo Dk Mwakyembe alihamishiwa Wizara ya Habari akitoka Sheria
baada ya Nape Nnauye kutenguliwa huku Profesa Kabudi ambaye ni Mbunge wa
Kuteuliwa akichukua nafasi ya Dk Mwakyembe.
Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri hao sambamba na mabalozi
wawili, Rais Magufuli aliwataka waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo hivyo
kuwa makini na kuepuka kuandika habari za uchochezi ambazo zinaweza kuiingiza nchi
pabaya.
“Waandishi kuweni waangalifu na kalamu zenu kwa sababu siku
Tanzania ikiingia kwenye machafuko na nyie mtakua sehemu ya watu waliochangia
kutokea kwa machafuko, angalieni nchi zote ambazo zilifikia pabaya chanzo
kilikuwa ni kalamu zetu, hata Rwanda mauaji ya kimbari yalichangiwa kwa kiasi
kikubwa na waandishi wav habari,” alionya.
“Hata mkiangalia magazeti yote ya leo (jana) yamejaza picha ya mtu
aliyefanya kosa moja tu na hata kurasa za ndani zimejaza habari hiyo hiyo,
kwani hakuna habari zingine za kuandika? Sasa Dk Mwakyembe nenda kasimamie kwa
umakini tasnia ya habari na kuchapa kazi, Serikali iko na wewe na siko tayari
kuona nchi ikichezewa,” alisema Rais Magufuli.
Alionya wamiliki kwa kuzipa uzito habari mbaya huku akitolea mfano
wa chombo kimoja cha televisheni kwamba kimekuwa kikirusha habari ya maandamano
ya wakulima au wafugaji kwa kuzipa kipaumbele na muda mrefu.
“Nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari kuweni makini na
angalieni, kama mlifikiri mna uhuru wa namna hiyo si kwa ukubwa huo, si kwa
utawala wangu, Mwakyembe nenda kapige kazi Serikali iko imara na kama kuna watu
walishindwa kuchukua hatua wewe nenda kachukue.
“Kuna vyombo vya habari vimetangaza kutoandika habari za mtu fulani,
wakati huo huo wanaandika mbaya tu, kama hamtaki kumwandika si msiandike
kabisa? Acheni kuandika yote mazuri na mabaya,” alisema Rais Magufuli akimaanisha
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyesusiwa na vyombo vya habari.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Dk Mwakyembe alimshukuru Rais kwa
kumwamini na kumpa wadhifa huo na kuahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uaminifu
mkubwa. Profesa Kabudi alisema shukrani za kipekee anazipeleka kwa Mwenyezi
Mungu kwa kumwezesha Rais kumpa nafasi hiyo kubwa na kuahidi kuifanya kwa nguvu
kubwa na uaminifu.
“Jana (juzi) na usiku ulikuwa mgumu sana kwangu, nimerudia kuisoma
Zaburi ya 15, inasema, ‘Nani ee Mwenyezi Mungu atakayekaa hemani mwako? Nani
atakaeishi juu ya mlima wako mtakatifu?’ Huku nikimwita Mungu anisaidie mimi na
wewe.
“Siwezi kuzungumza chochote kabla ya kuonana na wewe na uongozi wa
juu wa Serikali, kwani mkamia maji hayanywi, nami sitaki kuyakamia, niseme tu
ahsante Rais na ninakuahidi utumishi wa nguvu zangu zote,” aliahidi Profesa
Kabudi.
Katika hafla hiyo pia Rais Magufuli alimwapisha Dk Abdallah Possi
kuwa Balozi nchini Ujerumani, George Masima aliyepangiwa Israel na Sylvester
Mabumba kuwa balozi wa visiwa vya Comoro na Stella Mgasha kuwa Kamishna wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama.
0 comments:
Post a Comment