*Watendaji wapishana kauli kiwango cha dhahabu kinachosafirishwa nje ya nchi
*Acacia watangaza hasara Sh, bilioni 40
Fidelis Butahe
BUNGE limeingilia kati sakata la kuzuia makontena
282 yenye mchanga wenye dhahabu katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo Spika,
Job Ndugai ametangaza kuundwa kwa timu ya wabunge kuchunguza jambo hilo, pamoja
na kupitia mikataba yote ya madini.
Wakati hayo yakiendelea, Kampuni ya
Acacia inayoendesha migodi ya Buzwagi na Bulyang’ulu imetangaza kupitia
mkurugenzi wake, Brad Gordon kuwa tangu kuzuiwa kusafirishwa mchanga huo,
wamepata hasara ya takriban Sh bilioni 40.
Hatua hiyo ya Bunge inafuatia Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuzuia makontena 282 yenye mchanga wenye
dhahabu katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa amri ya Rais
John Magufuli kuzuia yasisafirishwe kwenda nje ya nchi.
Ndugai alitoa maelezo hayo jana baada ya
kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo akitokea mkoani Dodoma akimbatana
na wabunge 10 wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Bajeti, ambao
walihoji maswali yaliyozaa majibu yaliyotofautiana kutoka miongoni mwa
watendaji wa TPA na Wizara ya Nishati na Madini.
Wakati Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit
Kakoko akisema asilimia 90 ya mchanga huo una madini ya dhahabu, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Ntalikwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika walimpinga
na kueleza kuwa mchanga huo una kiasi kikubwa cha shaba na madini ya fedha.
“Kama mchanga huu una shaba zaidi mbona
hakuna hata kontena za Zambia hapa wakati nchi hiyo ndio inazalisha zaidi
shaba,” alihoji Ndugai huku Profesa Ntalikwa akitaka ufanyike uchunguzi zaidi
kujua ni madini gani yapo kwa wingi katika mchanga huo.
Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Dar
es Salaam, Terminal I, Ndugai alikwenda moja kwa moja bandarini na kufanya
kikao cha ndani, kabla ya kuanza kukagua makontena hayo yaliyokuwa yamegawanywa
katika maeneo matatu tofauti.
Katika msafara huo, Ndugai na wabunge
walishikwa na butwaa baada ya kuelezwa kuwa sampuli ya mchanga huo ikishapimwa
na TMAA, hakuna mtu yeyote anayehakiki zaidi ya mgodi husika na nchi
unapokwenda.
Siku nne zilizopita Rais John Magufuli
alishuhudia makontena 20 katika bandari hiyo yakiwa na mchanga wenye dhahabu, ambapo
aliagiza kutosafirishwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama.
Baada ya agizo hilo, juzi yalikamatwa
mengine 256 katika bandari hiyo na kufanya idadi yake kuwa 282 baada ya moja
kuongezeka jana kwa mujibu wa Kakoko.
Ilivyokuwa
Kakoko: Kontena zote zinapita kwenye
skana na kuna skana sita za kukagua kontena zitafungwa. Kwa sasa kontena zote
tunazozikamata tunaziweka alama ya X na zipo chini ya ulinzi na hapa kuna
kamera tunaona kila kitu kinachofanyika.
Ndugai: Mtu wa TMAA yuko wapi? Hivi
kontena ngapi zipo katika mgodi wa Buswagi na Bulyanhulu, ngapi zipo njiani na
ngapi zimeshafika hapa Dar es Salaam?
Mhandisi Shamika: Hapa sina takwimu
kamili zipo ofisini maana kontena zikisafirishwa mkaguzi wetu anakuwa na
takwimu zote.
Ndugai: Kwa wastani mnatoa kontena ngapi
kwa mwaka zinazosafirishwa?
Mhandisi Shamika: Kwa mwaka Buzwagi ni
kontena 24,000 na Bulyanhulu kontena 21,000. Wastani kwa mwaka zinakuwa kontena
55,000 hadi 60,000 za tani 20 kila moja.
Profesa Ntalikwa: Ili kujiridhisha na
taarifa za mali iliyopo kwenye kontena ni kutengeneza timu ya wataalam kuchukua
sampuli kupeleka maabara ili kuzipima. Timu hii ihusishe taasisi nyingine,
tukimaliza zoezi hilo tutaitoa taarifa ili kila mtu ajue.
Ndugai: Anayepima mchanga huu ni
mwajiliwa wa TMAA, hivi kuna mtu mwingine anayepima?
Mhandisi Shamika: Sampuli tunapima sisi
TMAA, mgodi wenyewe na pia huko nchi unakokwenda huu mchanga nao wanaupima ili
kujiridhisha na vipimo vyetu. Vipimo vyetu hupishana kidogo.
Ndugai: Kampuni za madini zimesajiliwa
Uingereza si ndio? Wazungu hao, kontena hizi zinaenda hukohuko kwa wazungu,
kwanini wewe TMAA usiwe na watu watatu zaidi ndani yako wa kujiridhisha na
vipimo? Hamdhani hawa wazungu wanaweza kukubaliana kutoa takwimu za uongo.
Mhandisi Shamika: Tumelichukua hilo
mheshimiwa. Ila dhahabu katika mchanga huu ni asilimia 0.02.
Kakoko: Tuna imani na hatuna wasiwasi
kuwa asilimia hizo za dhahabu sio zenyewe. Humu tuna dhahabu nyingi mno
asilimia 90. Katibu Mkuu ni mgeni anapokea taarifa tu. Tunataka kupata takwimu
za kuanzia Julai, tutawaandikia barua kesho (leo) asubuhi. Hivi mbona TRA hawakagui
hapa?
Profesa Ntalikwa: Tunataka usafishaji wa
mchanga kufanyika hapa nchini, tunatafuta mwekezi na ni zoezi tunaloendelea
nalo ili kupata mwekezaji.
Ndugai: Hivi mtu anaweza kuwekeza eneo
la dhahabu lenye asilimia 0.02 kweli?
Mhandisi Shamika: Kwa asilimia hiyo
mwekezaji hawezi kuwekeza.
Ndugai: Kama hawezi, iweje achukue
asilimia 0.02 ya kiwango cha dhahabu asafirishe na kuingia gharama mpaka Japan
(kicheko). Hili tuliache hivi hivi.
Mhandisi Shamika: Shaba ni asilimia 17
na dhahabu ni asilimia 0.02, na madini ya fedha ni 0.02 huyu ni mfanyabiashara
anataka kupata vitu vyote vitatu.
Kauli ya Ndugai
“Tukienda bungeni tutatangaza hatua
tutakazochukua. Ila kwanza tutaunda timu ya wabunge na itachunguza jambo hili
kuanzia mgodini hadi kwenye usafirishaji,” alisema Ndugai.
“Tunataka kujua biashara hii inaendeshwa
na nani na nani anayefaidika. Tutataka kujua katika madini watanzania
wananufaika vipi maana tangu mwaka 1998 kontena 50,000 zinasafirishwa kwa mwaka
kwenda nje.”
Alisema haiingii akilini tangu kipindi
hicho hadi sasa kiwango cha dhahabu kinachosafirishwa kiwe asilimia 0.02 katika
kila kontena lenye mchanga huo.
“Tutaipitia mikataba ya madini yote ili
kujua nini kilichomo humo na tutachukua jukumu la kuishauri Serikali. Tunataka kujua
nani anasimamia maslahi yetu huko mchanga unapokwenda,” alisema Ndugai.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania
kuchukua hatua kwa madai kuwa utajiri wan chi unaondoka kila uchwao.
0 comments:
Post a Comment