Celina Mathew
Ibrahim Lipumba |
MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, ametangaza rasmi kuwa nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho ya Maalim
Seif Sharrif Hamad itakaimiwa na Magdalena Sakaya kutokana na kushindwa kutimiza
majukumu yake ipasavyo.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana,
wakati akitoa maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
kilichofanyika Machi 25 na 26.
Profesa Lipumba alisema Baraza hilo
limesikitishwa na kukasirishwa na vitendo vya Maalim kuhujumu chama na kupandikiza
chuki, uhasidi na uhasama dhidi yake, hasa miongoni mwa wanachama wa CUF
Zanzibar.
“Tangu Septemba mwaka jana, Katibu Mkuu
hajafika ofisi kuu za chama amekaidi mwito wa Mwenyekiti wa kuja ofisi kuu
kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.
“Baraza Kuu limeagiza kuwa Katiba ya CUF
ya mwaka 1992 toleo la 2014 ibara ya 93 (3) ambayo inaeleza Katibu Mkuu
anapokuwa nje ya nchi au atakaposhindwa kufanya kazi zake kwa sababu yoyote
ile, Naibu Katibu Mkuu anayemfuata kwa madaraka, atakaimu ukatibu mkuu hadi
atakapokuwa tayari kuendelea na majukumu, iheshimiwe na kutekelezwa,” alisema.
Alisema Baraza limejiridhisha kuwa
Katibu Mkuu ameshindwa kutimiza majukumu yake na kwa kuzingatia Katiba, Baraza linatangaza
rasmi kuwa Sakaya ndiye anayemfuata Maalim kwa madaraka na atafanya kazi zote
za Katibu Mkuu.
Aidha, aliziarifu ofisi za CUF za wilaya
na asasi zote kuwa mawasiliano yote kuhusu masuala ya chama yawasilishwe kwa
Sakaya katika ofisi za Buguruni, Dar es Salaam na kwamba zinazotolewa na Maalim
zipuuzwe.
Ashangazwa
Wakati huo huo, alisema Baraza hilo
linashangazwa na Maalim Seif kujenga urafiki na Waziri Mkuu mstaafu Frederick
Sumaye akiwa ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Serikali iliyotekeleza
operesheni ya kusababisha mauaji ya wanachama wa CUF kwenye maandamano ya
Januari 26 na 27, 2001.
“Katibu Mkuu anasahau mauaji hayo na
anamfanya Sumaye swahiba wake wa karibu
na alitangaza hadharani kwamba kama kiongozi wa Chadema nia yake ni kuhakikisha
Tanzania ina vyama viwili (CCM na Chadema), ni wazi kwamba lengo lao ni kuiua
CUF kwa manufaa ya chama chake,” alisema.
Alimtaka Maalim kuacha mkakati wa kuiua
CUF Bara ili kuistawisha Chadema kwa kisingizio cha Ukawa.
Aliongeza kuwa kwa sasa safari zote za
chama zinaratibiwa na Sakaya au wasaidizi wake na kumwagiza Maalim asifanye
ziara yoyote ya chama Bara kwa kuwa Baraza limejiridhisha kwamba kwa sasa
mpango wake ni kukihujumu kwa kushirikiana na viongozi wa nje.
Kuhojiwa
Profesa Lipumba aliongeza kuwa Baraza limeteua
wajumbe watatu wa Kamati ya Maadili, ambao ni Mashaka Njole, Hamis Hassan na
Rukhia Kassim ambao wataungana na waliotajwa kwenye Katiba ibara ya 99 kifungu
cha (2)(i-v) ambayo itawaita Maalim na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor
Mazrui na kuwahoji.
Alisema Maalim Seif atahojiwa kwa kushindwa
kutimiza majukumu yake kwa kutofika kwenye ofisi za chama hicho na kukaidi mwito
wa Profesa Lipumba ambaye ndiyo Mwenyekiti ili kupewa maelekezo ya kuandaa
vikao vya chama.
Pia Mazrui ataitwa kuhojiwa kwa kutoa
kauli za dharau na kejeli dhidi ya Mwenyekiti na wabunge wawili waliofanya
hujuma kwa kuacha kumnadi mgombea udiwani wa CUF wa kata ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro
na badala yake wakamnadi mgombea wa Chadema.
Alisema mbunge mwingine ni
aliyemshawishi mgombea udiwani wa CUF kata ya Kiwani, Muleba kuhama chama na
kugombea udiwani kupitia Chadema.
Wagombea EALA
Pia Baraza hilo lilipokea majina saba ya
wanachama waliojitokeza kugombea ubunge wa Afrika Mashariki ambao ni Mneke
Jaafar, Khalifa Khalifa, Zainabu Mndolwa, Dadi Hemed, Thomas Malima, Mohammed
Mnyaa na Sonia Magogo.
Alisema Baraza lilizingatia kanuni za
uchaguzi wa wabunge wa jumuiya hiyo na kuteua majina matatu ambayo
walikubaliana mmoja awe mwanamke, mwingine atoke Zanzibar na aliyebaki atoke Bara.
Profesa Lipumba alisema baada ya
majadiliano, Baraza Kuu liliteua wagombea watatu ambao ni Magogo, Mnyaa na
Malima.
Bodi mpya
Aidha, Baraza liliteua wajumbe wa Bodi
mpya ambao ni Peter Malebo, Abdul Magomba, Hajra Silia, Amina Thomas na Aziz
Dagesh kutoka Bara na Salha Hilal, Asha Said, Suleiman Issa na Mussa Kombo
kutoka Zanzibar.
Aliagiza Bodi kufuatilia fedha za ruzuku
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ili ipatikane na kuendeleza shughuli za ujenzi
wa chama na kuhakikisha akaunti zote zilizositishwa na Maalim zinafunguliwa.
Pia kufuatilia kesi zilizofunguliwa kwa
jina la chama kama zina tija kwa chama na kufuatilia hali ya miradi
iliyoanzishwa na chama maeneo mbalimbali nchini na kuwasilisha taarifa zake
kwenye kikao cha Bodi.
Nafasi wazi
Baraza hilo lilijaza nafasi zilizokuwa
wazi kwa kutumia mapendekezo yaliyopelekwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa
kuwapitisha Abeid Mlapakolo kutoka kanda ya Pwani kuwa mjumbe akichukua nafasi
ya marehemu Ashura Mustapha.
Wengine ni Martha Haule kutoka Kanda ya
Ziwa kuchukua nafasi ya Mkiwa Kimwanga aliyehama chama mwaka juzi, Dauda Hassan
kutoka Kanda ya Kati kuchukua nafasi ya Chifu Lutalosa Yemba aliyevuliwa
uanachama na Baraza.
Pia Juma Nindi kuchukua nafasi ya Lobora
Ndarapoi aliyehama chama mwaka 2015 na Maisara Mshamu kutoka Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini anayechukua nafasi ya Mohammed Khalifa aliyehama chama mwaka juzi.
Wakurugenzi
Baraza lilithibitisha kwa kauli moja
uteuzi wa Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge ambaye pia anakaimu
nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, Nassor Seif, Naibu
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge Mneke Jaafar, Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Uhusiano na Umma, Abdul Kambaya.
Wengine ni Mkurugenzi wa Fedha na
Uchumi, Thomas Malima, Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi na Kaimu Naibu Mkurugenzi
wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Maftaha
Nachuma.
Aidha, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Khalifa Khalifa, Naibu
Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Masoud Mhina na Mkurugenzi wa Haki za
Binadamu na Sheria, Zainab Mndolwa.
“Wajumbe hawa ndio wanaounda Kamati ya Utendaji
mpya itakayofanya kazi za chama ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini
ya uongozi wa Kaimu Katibu Mkuu Sakaya,” alisema Profesa Lipumba.
0 comments:
Post a Comment