Charity James
TIMU ya Simba SC, imesema ipo katika mpango wa kuhakikisha
inavunja rekodi katika viwanja vya mikoani ambavyo wamekuwa wakishindwa kupata
matokeo mazuri lengo likiwa ni kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kutwaa ubingwa.
Simba inatarajia kushuka uwanjani Aprili 2, mwaka huu kuumana na
Mbao FC ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo katika mwendelezo wa mechi za Ligi
Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kisha kucheza na
Toto Africans.
Katika miaka ya hivi karibuni, Simba imekuwa haina matokeo mazuri
ukanda huo hasa katika mechi zake inazocheza Kirumba na Toto African imekuwa
ndio kikwazo kwa timu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja,
alisema wao wamekusudia kutwaa ubingwa msimu huu, hivyo wapo tayari kung’oa
visiki vyote ili kuhakikisha wanafanya vizuri.
“Tumechoka kuendeleza uteja katika viwanja vyote ambavyo tumekuwa
tukipoteza alama muhimu, hivyo hatuko tayari kupoteza ubingwa tunaoutamani kwa
muda kisa kupoteza alama nyingi Kanda ya Ziwa,” alisema.
Akizungumzia mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Madini FC ambapo
waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Laudit Mavugo, alisema
wanawashukuru wachezaji kwa kufanya kile walichotumwa na mwalimu na kuisaidia
timu kuingia katika hatua ya nusu fainali.
Alisema kumekuwa na maneno mengi kuwa safu yao ya ushambuliaji ni
butu na kusababisha kupata mabao machache katika michezo yao mbalimbali,
kikubwa nni kupata ushindi kwanza na kupata idadi kubwa ya mabao hiyo ni kazi nyingine.
“Ligi ilisimama kwa muda na inatarajiwa kuanza, hivyo mashabiki na
wapenzi wa Simba wasife moyo na washambuliaji wetu wapo katika nafasi nzuri ya
kufunga idadi kubwa ya mabao na yataweza kutusaidia kuhakikisha tunatwaa
ubingwa kama tulivyojipangia,” alisema.
Alisema wapinzani wao wasitarajie kuwa idadi kubwa ya mabao waliyonayo
ndio itawasaidia kutwaa ubingwa msimu huu wao bado wana nafasi ya kuongeza
idadi ya mabao hayo na pia katika suala la alama kwao haliwapi tabu kwasababu wana
imani ya kufanya vizuri katika michezo iliyobaki.
0 comments:
Post a Comment