Magendela Hamisi
CHAMA cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kimesema hakukuwa sababu
ya kutoitwa kwa wachezaji wao kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa
ajili ya kujiandaa na michezo ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa
wachezaji wa ndani (CHAN) na Mataifa ya Afrika (AFCON).
Akizungumza juzi, Ofisa Habari wa chama hicho, Ally Bakari
‘Cheupe’ alisema hawaoni sababu za msingi kwa wachezaji wa visiwa hivyo
kutojumuishwa kwenye kikosi hicho na kufafanua kuwa hali hiyo imekuwa
ikijitokeza mara kadhaa.
Alisema sababu iliyotolewa wa Kocha Salum Mayanga wakati
akitangaza kikosi hicho, kwamba wachezaji wa Zanzibar wameachwa ili kusikilizia
hatima ya ZFA kujiunga na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) haina
msingi kwa sasa.
“Nasema hivyo (kuhusu kuachwa wachezaji wa Zanzibar) kwa kuwa
ratiba ya makundi ya mashindano hayo imeshatangazwa, hivyo hata kama ZFA ikipitishwa
kujiunga na CAF hakika kwetu kutakuwa na changamoto ya kushiriki katika
michuano hiyo labda katika mashindano yajayo,” alisema.
Alisema anaamini bado wachezaji wa Zanzibar walikuwa na nafasi ya
kuitwa katika kikosi kilichotangazwa mwanzoni mwa wiki hii na Kocha Mkuu
Mayanga kwa ajili ya kushirikiana na wenzao wa Tanzania Bara kutafuta nafasi ya
kushiriki michuano hiyo.
Alisema pamoja na dosari ya kuachwa kwa wachezaji wa Zanzibar,
kwani waliochaguliwa wapo kwa ajili ya kujenga nyumba moja wao hawana kinyongo,
wanawaombea Mungu ili wafanikiwe katika dhamira iliyopo mbele yao.
Mwanzoni mwa wiki kocha Mayanga aliita wachezaji 26 kujiunga na
kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ bila wachezaji wa Zanzibar akisema
inatokana kusubiri uamuzi wa kikao cha CAF kitakachofanyika leo mjini Adis
Ababa, Ethiopia kuhusu kuipa uanachama Zanzibar.
Kikosi cha Taifa Stars kinatarajiwa kuingia kambini Machi 19 mwaka
huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa zilizopo
kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa).
Pia baada ya kutangaza kikosi hicho Mayanga, alisema timu hiyo
itacheza mechi mbili za kujipima nguvu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
dhidi ya Botswana Machi 25 na Burundi Machi 28 kwa ajili ya maandalizi ya AFCON
na CHAN.
Taifa Stars imepangwa kucheza na Rwanda katika mchezo wa michuano
ya CHAN Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya
kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
Ikiitoa Rwanda, Tanzania itacheza na mshindi kati ya Uganda na
Sudan Kusini au Somalia katika raundi ya tatu, mechi ya kwanza itachezwa kati
ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
Tanzania ilishiriki mara moja fainali za CHAN mwaka 2009
zilipozifanyika kwa mara ya kwanza kabisa. Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars
imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja fainali za AFCON 2019,
wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi
ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora.
Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980
nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi.
0 comments:
Post a Comment