*Matendo, kauli zake zasababisha mkanganyiko
*Sifa anazopewa na Rais sasa zaibua mjadala mkali
*Sifa anazopewa na Rais sasa zaibua mjadala mkali
Waandishi Wetu
Paul Makonda |
NI wazi kuwa tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda zinaigonganisha mihimili ya Dola na kuzua sintofahamu miongoni mwa
wateule wa Rais John Magufuli.
Tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda
ametoa kauli tata akituhumiwa katika mambo tofauti na kufanya vitendo
vilivyozua mjadala jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na
gazeti hili, wametaja athari zinazoweza kutokea iwapo mamlaka hazitachukua hatua.
“Inawezekana Rais John Magufuli ana vyanzo vyake
vinavyompa habari hivyo anajua utendaji na hatua zote zinazofanywa na mteule
wake huyo.
Athari zinaweza kutokea iwapo Rais atashindwa kuchukua
hatua za kinidhamu, maana wananchi wanajua na kuona na wanasubiri hatua
zichukuliwe,” alisema Hamad Salim, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT).
Ijumaa iliyopita, Makonda anayetajwa kuivuruga mihimili
mitatu ya Dola; Serikali, Bunge na Mahakama aliingia studio za Clouds TV usiku
akiwa na askari na silaha za moto, tukio ambalo lilithibitishwa na Mkurugenzi
wa Vipindi na Uendeshaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.
Ruge alisema Makonda aliingia studio kuchukua kinguvu
sehemu ya kipindi cha Shilawadu kilichokuwa kimezuiwa kurushwa kutokana na
kutokidhi matakwa ya kitaaluma, kikimhusisha mwanamke anayedaiwa kuwa mzazi
mwenzake na hasimu wa Makonda, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima.
Makonda pia anahusishwa na mtu anayeitwa Daudi Bashite
aliyesoma Shule ya Msingi Koromije na Sekondari ya Pamba na kumaliza kidato cha
nne na kupata daraja la sifuri kabla ya kughushi cheti na kuendelea na elimu ya
juu.
Mkuu huyo wa mkoa pia anatakiwa kwenda kujieleza kwenye Kamati
ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, akituhumiwa kukashifu wabunge kuwa wakati
mwingine hukosa cha kuzungumza na ndiyo maana husinzia bungeni.
Tukio la juzi la Clouds lilimfanya Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuunda kamati ya kulichunguza na kutoa
majibu ndani ya saa 24, huku wadau wa habari wakitoa kauli za kupinga kuvamiwa
kwa ofisi za Clouds kwa maelezo kuwa ni kuminya uhuru wa vyombo vya habari.
Licha ya tuhuma hizo, Rais Magufuli juzi alitumia
ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za
Sam Nujoma na Morogoro jijini hapa, kumtaka mkuu huyo wa mkoa kuchapa kazi na
kutosikiliza habari alizoziita kuwa ni za mtandaoni na udaku.
Wachambuzi Katika ufafanuzi zaidi, Hamad alisema:
“Kitendo cha kuvamia chombo cha habari si cha kiungwana, nafikiri Rais alipaswa
kutumia busara zaidi katika kulizungumzia hili, kwa sababu kama mteule wake
anaandamwa na kashfa kila kukicha na yeye hachukui hatua, basi wananchi
wanaweza kuuchoka utawala wake.”
Aliongeza: “Kumsifia sana kunaweza kuzaa tafsiri mbaya
kwa wananchi, wengine wanaweza kudhani kuna mkono wake katika hili na ndiyo
maana inampa ugumu kuchukua hatua. Kimsingi Rais ataharibu taswira nzuri ambayo
alishaanza kujijengea.”
Alibainisha kuwa kauli ya Rais Magufuli kuwa watu wenye
akili ndogo hujikita katika kuzungumzia maisha binafsi ya watu, ni sawa na
kutukana wananchi kwa maelezo kuwa wananchi kuhoji cheti cha Makonda ni haki
yao.
“Wapo ndugu na jamaa zao ambao wamepoteza ajira kwa
kughushi vyeti, sasa wanaposikia mkuu wao wa mkoa ana tuhuma kama hizo, lazima
wahoji. Ni kama Nape anataka kuchukua hatua lakini Rais anaonekana kuwa na
imani na Makonda,” alisema Hamad.
“Mfano matamko yanayotolewa na Makonda… anaonekana kuwa juu
ya sheria na hakuna wa kumfanya lolote. Hii inachafua sura ya Serikali kwa
sababu viongozi wanaonekana kuvunja sheria na bado Rais anawasifia.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema mambo yanayofanywa na
Makonda ni kinyume na maadili na mwongozo wa Sheria ya Utumishi wa Umma.
“Ni kuishushia heshima Serikali na kuwafanya wananchi
kupata shaka nayo. Rais kumsifia Makonda licha ya kuandamwa na tuhuma kibao
ukiwamo uvamizi ni sawa na kuhalalisha tabia hiyo kwa viongozi wengine wa
Serikali ambao sasa wanaweza kufanya kama alivyofanya Makonda,” alisema Dk
Kyauke.
Hata hivyo, mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Benson
Bana alihoji sababu za kuibuka kwa tuhuma za Makonda sasa, si wakati akiwa Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni.
“Makonda amekuwa mfano wa kuigwa kwa wakuu wengine wa
mkoa kutokana na ufanisi wake wa kazi. Inawezekana yanayosemwa kuhusu yeye ni
kutokana na vita aliyoianzisha dhidi ya dawa za kulevya,” alisema.
Kauli ya Dk Bana ilipingwa na Mbunge wa Kaliua, Magdalena
Sakaya (CUF) na kubainisha kuwa Rais kumkingia kifua Makonda kutaifanya nchi
kuingia kwenye mgogoro na mashirika ya kimataifa kwa kuingilia uhuru wa vyombo
vya habari.
“Kauli ya Magufuli dhidi ya Makonda jana (juzi) ni mbaya
kwa Taifa kwa sababu inachukua sura ya Rais na kufuta mazuri yote aliyofanya
hadi sasa. Makonda mwenyewe atashusha heshima yake na kuonekana kila
analolifanya lina baraka kutoka Mamlaka ya juu,” alisema Sakaya.
0 comments:
Post a Comment