Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema ipo katika hatua za
mwisho kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa ya kisasa itakayokuwa
na uwezo wa kuchukua tani 300 za mizigo, magari 25 na madaraja matatu kwa ajili
ya sehemu ya kukaa abiria.
Aidha, imesema haitavumilia wala kusita
kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya
barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari baada
ya kukagua Bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema utekelezaji wa mradi huo umechelewa
kutokana na kukosa sifa kwa makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili
ya kutekeleza mradi huo wa ujenzi.
“Nataka kujenga meli ya kisasa ili
kuweza kufupisha safari kutoka masaa 10 hadi matano kutoka Bukoba hadi Mwanza, hivyo
kufanya usafiri wa majini kuwa wa kuaminika na salama”, alisema Mbarawa.
Aidha, alifafanua kuwa kutokana na
utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia kuleta wafanyakazi makini kwa ajili
ya kupitia taarifa za kifedha na usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya
Ziwa, Abel Moyo aliiomba Serikali kufanya ukarabati wa meli nchini hasa
zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha wanazozipata wakazi wa mikoa
hiyo.
Katika hatua nyingine, Mbarawa amekagua
Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi kupeleka wakaguzi wa ndani kwa ajili ya
kukagua na kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa
na watendaji.
“Tunataka Posta iwe safi na kupunguza
changamoto zinazoikabili kwani ni Shirika kubwa na lenye rasilimali nyingi
ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua mapato ya shirika”, alisisitiza.
Aidha, Mbarawa ameagiza Wakala wa Ufundi
na Umeme (Temesa), kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika utengenezaji
wa magari yanayokuja kupata huduma katika karakana yao.
Kwa upande wake, Meneja wa Temesa Mhandisi
Zephrine Bahyona amemuomba waziri kusaidia kusisitiza taasisi za Serikali
kupeleka magari yao kwenye karakana zao na kulipa madeni kwa wakati ili
kupunguzia Wakala huo mzigo wa madeni kutoka katika taasisi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari
wilayani Karagwe, mkoani Kagera baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene
yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana
ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
"Najua bado kuna watu wanaendelea
kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea
kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria", amesema Profesa
Mbarawa.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo,
Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU),
kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kwa kusimamia ujenzi
wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango.
0 comments:
Post a Comment