Fidelis Butahe
Dk. Shein na Dk. Magufuli Ikulu Dar es Salaam |
SIKU 15 baada ya Rais John Magufuli kuliagiza Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kuwakatia umeme wadaiwa wote ili wapate fedha za kuendesha
shirika hilo kwa maendeleo ya Taifa, ikiwamo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
inayodaiwa Sh. bilioni 121, hatimaye Serikali hiyo imeanza kulipa deni.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Machi 6 mwaka huu wakati akiweka
jiwe la msingi katika kituo cha kupoza umeme cha njia ya Kv 132 mkoani Mtwara.
Siku tatu baada ya kauli hiyo ya Rais, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Tanesco, Dk. Tito Mwinuka alitoa siku 14 kwa Zeco, wizara na taasisi za
Serikali kulipa madeni hayo kabla ya kukatiwa huduma.
Lakini jana, wakati ikiwa zimebaki siku nne kabla Tanesco
haijaanza utekelezaji wa operesheni hiyo, Ikulu ilitoa taarifa ikieleza jinsi
Rais Magufuli alivyokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein na maofisa waandamizi wa Tanesco walioongozwa na Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye aliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar
kuwa hawatakatiwa umeme.
“Waziri wa Nishati na Madini amewatoa hofu wananchi wa Zanzibar
kuwa hawatakatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanza kulipa
deni inalodaiwa na Tanesco,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ikimnukuu Profesa Muhongo.
“Tayari SMZ imeanza kulipa kiasi cha Sh bilioni 10 na itaendelea kulipa
deni hilo mpaka litakapomalizika.”
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Profesa Muhongo alitoa wito kwa wadaiwa
wote wa Tanesco kulipa madeni yao katika kipindi cha siku tano (mpaka kufikia
jana) zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme.
Baada ya Tanesco kutoa siku 14, Dk Shein alizungumza na waandishi
wa habari alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume,
akitokea nchini Indonesia katika mkutano maalumu ulikomwakilisha Rais Magufuli na
kusema kama nishati hiyo ikikatwa, watatumia vibatari kupata mwanga.
“Naamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Serikali
ya kiungwana, inayojali watu wake, hivyo haiwezi kufanya hivyo kwenye suala
hili la kuzima umeme visiwani Zanzibar na iwapo ikitokea umezimwa, Zanzibar
watakuwa tayari kurudi kwenye matumizi ya vibatari,” alisema Dk Shein.
Katika maelezo yake ya Machi 9, Dk. Mwinuka alisema kitendo cha
Tanesco kudai kiasi kikubwa cha fedha kunachangia kurudisha nyuma utendaji wa
shirika hilo katika kusambaza huduma ya umeme nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo, baada ya muda waliotoa kwisha bila
deni hilo kulipwa, Tanesco itachukua uamuzi mgumu wa kuwakatia umeme wadaiwa
hao.
Alibainisha kuwa katika deni hilo, Zeco inadaiwa Sh bilioni 127, mashirika
ya Serikali, wizara na taasisi Sh bilioni 52, huku kampuni binafsi na wateja
wadogo wakidaiwa Sh bilioni 94.
0 comments:
Post a Comment