*Azungumzia aliyemwonesha Nape bastola Dar es Salaam
*Ataka atimuliwe kisha ashitakiwe pamoja
na waliomtuma
Mwandishi Wetu
Tundu Lissu |
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema Bunge linalazimika
kuunda tume ya kuchunguza walinzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
Alisema hayo katika taarifa yake kwenye
mitandao ya kijamii jana akibainisha kuwa iwapo mlinzi aliyemtisha kwa bastola aliyekuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitoka Idara ya
Usalama wa Taifa (TISS) ni kosa kisheria.
“Nimeona taarifa kwamba mtu aliyemtolea
Nape bastola majuzi ni mlinzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni ofisa wa
TISS, kama taarifa hizi ni za kweli, basi mtu huyo anapaswa kufukuzwa kazi mara
moja, kukamatwa na kushitakiwa kijinai,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha
TISS, maofisa usalama wa taifa wamekatazwa kufanya kazi za kipolisi kama kukamata
wahalifu, kuhoji watuhumiwa na kufanya upelelezi wa kijinai.
Lissu alisema alichokifanya kumzuia Nape
kuzungumza na waandishi wa habari kwa kumtishia bastola kinaangukia majukumu ya
kipolisi ambayo TISS haina mamlaka nayo kwa mujibu wa sheria.
“Kikubwa na muhimu zaidi ni hiki: huyu
askari wa TISS alikuwa anafanya kazi kwa maagizo au maelekezo au amri ya nani?”
Alihoji.
Rais huyo wa TLS alisema kama alikuwa
anatekeleza maagizo ya bosi wake yaani Mkuu wa Mkoa au bosi mwingine, hao nao
wanapaswa kufukuzwa kazi na kushitakiwa kijinai.
Mbunge huyo alisema kama ni maagizo ya
Rais John Magufuli kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, basi hiyo ni fursa ya
mashitaka ya Bunge dhidi ya Rais.
Alisema jambo hilo ni kubwa linalohitaji
kuundiwa kamati teule ya Bunge kulichunguza na kuchunguza mazingira yote yanayomzunguka
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na matumizi yake ya askari wa vikosi vya ulinzi
na usalama.
Lissu alisema Mkuu wa Mkoa huyo
anaelekea kuamini kwamba ana uwezo wa kutumia askari atakavyo yeye binafsi.
“Anatakiwa kuondolewa mawazo hayo ya
kijinga kabla hajafanya jambo kubwa na baya zaidi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment