Mary Mtuka
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),
umetaka Watanzania kupuuza taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa
Mfuko huo uko hoi kiasi cha kushindwa kutoa huduma kwa wanachama wake.
Akikanusha madai ya taarifa hizo za
upotoshaji Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard
Konga alisema taarifa hizo ni upotoshaji wa hali ya juu na ni vema zikapuuzwa
huku akiwahakikishia Watanzania kuwa Mfuko uko imara na unatoa huduma kama
kawaida.
Alifafanua kuwa taarifa hizo zilianza
kutolewa na mtandao wa kijamii wa Jamii Forums na kusambaa kwenye mitandao
mingine.Taarifa hiyo ya upotoshaji ilikuwa inadai hivi: "NHIF hoi, watunga
muswada kuinusuru, mashirika makubwa kama Tanesco, BoT, TRA, TPA, kujiunga kwa
lazima.
"Taarifa hiyo si ya kweli na imejaa
upotoshaji kwa umma.Tunaomba mzipuuze, Mfuko wetu uko imara na unaendelea kutoa
huduma kama kawaida yake," alisema.
Akijibu hoja ya kwamba Mfuko uko hoi na
umeshindwa kuwalipa watoa huduma wake, alisema si za kweli na mtandao huo
ulikuwa na lengo la kupotosha umma.
Kuhusu madai ya ucheleweshaji ulipaji
madai kwa kukosa fedha na kusababisha wanachama kunyimwa huduma, alisema kwa
mujibu wa sheria ya Mfuko, malipo kwa
watoa huduma waliosajiliwa yanatakiwa kulipwa ndani ya siku 60 tangu
kuwasilishwa kwake na lengo la kufanya hivyo ni kuhakiki uhalali wa madai yaliyowasilishwa.
Akizungumzia madai ya wigo mdogo wa
huduma zitolewazo kwa wanachama, alisema Mfuko umeendelea kufanya maboresho kwenye
kitita cha mafao yatolewayo kwa wanufaika, kwa kuzingatia maoni ya wadau wake
wakiwamo wanachama, watoa huduma na waajiri.
Kuhusu madai ya kuwasilisha Muswada bungeni
kulazimisha mashirika makubwa kujiunga na Mfuko huo, alisema sheria ya Mfuko
inaelekeza watumishi wote wa umma, walio katika wizara, idara, taasisi na
mashirika ya umma, kujiunga kwa kuchangia asilimia tatu ya mshahara na mwajiri
naye anachangia asilimia tatu.
0 comments:
Post a Comment