Ibrahim Kunoga, Tanga
Mussa Mbarouk |
MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CUF), Mussa Mbarouk, amefichua
siri ya madiwani wa chama hicho kulegeza msimamo wao na kuamua kuingia kwenye vikao
vya Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo.
Sababu kubwa ya kulegeza msimamo wao ni baada ya kupewa
baraka na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza wa hadhara
uliofanyika uwanja wa Tangamano,Mbunge huyo ambaye awali alikuwa amezuiwa
kufanya mikutano hiyo alisema Katibu wa o mkuu ndiye aliyetoa baraka ili
kusukuma maendeleo ya wananchi.
“Katibu wetu mkuu alituita na kuwataka madiwani wa Jiji
la Tanga kuingia katika vikao vya baraza kwa sababu kuendelea kugoma ni
kusababisha kudodora maendeleo ya wananchi,” alisema Mbarouk.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho madiwani
wa CUF waligoma kuingia katika vikao vya baraza hilo, miradi mingi ilikwama na kama
wasingebadili msimamo, Benki ya Dunia ingesitisha msaada wa zaidi ya dola za
Marekani milioni 500.
Mbunge huyo alisema katika kipindi kifupi ambacho
madiwani hao kukubali kuhudhuria vikao, miradi mingi ya maendeleo imeanza
kutekelezwa ikiwamo ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami.
“Tanga tumeamua kuacha tofauti zetu za vyama, madiwani
tumeungana kwa ajili ya maendeleo na tunataka Tanga ikimbie,” alisema mbunge.
Awali, madiwani wa kata mbalimbali walieleza miradi
iliyotekelezwa katika maeneo yao na mikakati iliyopo ya kuhakikisha sekta ya
elimu, afya, maji, barabara na masuala ya kijamii inaendelezwa.
0 comments:
Post a Comment