Salha Mohamed
NEEMA Wambura (32)
aliyeungua kwa kumwagiwa maji ya moto na mumewe ameruhusiwa kutoka hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) huku akitoa ujumbe mzito kwa wanawake wanaotarajia
kuolewa.
Tukio hilo
lilitokea katika kijiji cha Kyagata, Tarime mkoani Mara, baada ya kuchuma
mahindi mawili na kuchoma ndipo akaadhibiwa na mumewe huyo huku akiwa na mimba
ya miezi minne.
Akizungumza
jana hospitalini hapo, Neema alisema kwa sasa amepona huku akiwashukuru
madaktari wa hospitali hiyo na Rais John Magufuli kwa msaada wake kwake.
Alisema
wanawake wanapotaka kuolewa waangalie wa kuwaoa ili yasiwakute kama yaliyomkuta
yeye, hadi kumwagiwa maji ya moto.
"Mimi
ungenikuta pale madhabahuni tunafunga ndoa usingeamini kuwa angenifanya hivi,
ni mwanamume aliyekuja kunichumbia akiniambia dada nakupenda na mimi
nikakubali, lakini sasa sina matiti," alisema.
Alisema baada
ya kumwagiwa maji ya moto alifungiwa ndani na alikwenda kuomba msaada kwa
wazazi wake wakamrudisha kwani walishakula mahari.
Alisema
alipata msaada wa kufika MNH huku akiwa na hofu ya kutopona akaendelea na
matibabu huku viungo vyake vikiwa vimeathirika na moto.
Neema alisema
alipata msaada wa matibabu kutoka kwa Rais Magufuli hadi kupona, kwani hata
shingo yake ilikuwa haigeuki vema.
"Nilikuwa
nasikia maumivu ya kidonda kama kunawaka moto kwa ndani hadi natamani nivue nguo
nitupe lakini baada ya Rais kupata taarifa suala hili lilimgusa," alisema.
Aliomba Mungu
amsaidie Rais Magufuli na amwepushe na mambo mabaya kutokana na ukarimu
aliomfanyia kwa kuokoa maisha yake.
Alisema hadi
sasa hajui aliko mumewe baada ya kumdhuru na huku
ndugu na wazazi wake wakimtenga.
Mkuu wa Idara
ya Upasuaji MNH, Dk Ibrahim Mkoma alisema walimpokea Neema Julai 6, mwaka juzi
akiwa amepewa rufaa kutoka hospitali ya Mkoa wa Mara.
"Alikuwa
na jeraha kubwa karibu kifua chote, shingo na kidevu kilikuwa kimeshikana,
mkono wa kushoto umeshikana na kifua," alisema.
Alisema baada
ya kumfanyia uchunguzi, tulibaini anahitaji upasuaji ambapo wa mwanzo
tulimfanyia Julai 21, 2015 iliyotenganisha shingo na kifua na kutenganisha
mkono wa kushoto kutoka kifuani na kufunika kidonda.
Dk Mkoma
alisema walichukua ngozi mapajani na baada ya mwezi ngozi bado haikushika vema
hadi shingoni, kidevuni na kwapa la kushoto.
"Agosti
tulimrudisha chumba cha upasuaji kumpasua sehemu ambayo haikushika vizuri
lakini akawa anaendelea vema na hakuwa na kidonda na shingo alikuwa anaweza
kunyanyua," alisema.
Alisema Desemba
2015 walimfanyia upasuaji wa tatu wakati huo wakichukua ngozi tumboni na kuweka
shingoni ili aweze kuzungusha shingo.
Februari mwaka
huu alikuwa anahisi kuumwa mkono na majeraha kuuma na alifika MNH na kupata
matibabu huku Rais akitoa msaada.
Alisema Neema
aliathirika kisaikolojia na hata kumsababishia kilema cha kudumu kwenye mkono
wa kulia kutokana na tishu kuharibika kwa moto.
"Rais
ameonesha mfano, watu waige alichokifanya kuanzia kwa mtu binafsi hadi jamii,Watanzania
wazuie mambo kama haya kutokea katika jamii zao," alisema.
Alisema jamii
inapaswa kupewa elimu ya namna ya kulinda haki za raia hasa wanawake, ili kuepusha
yaliyotokea kwa Neema.
0 comments:
Post a Comment