Waandishi Wetu
Paul Makonda |
TANGU gazeti hili lilipochapisha kwa mara ya kwanza
tuhuma za utata wa elimu ya Paul Makonda, zimepita siku 32 za mjadala mkubwa
kuhusu jina la Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mjadala huo uliotokana na kauli na matendo yake tangu
kuibuliwa kwa tuhuma hizo na zingine nyingi, ulifikia ukomo jana baada ya
vyombo vya habari kutangaza marufuku ya kutochapisha au kutangaza habari
zinazomhusisha kiongozi huyo wa mkoa.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Klabu ya Waandishi
wa Habari Dar es Salaam jana walikutana na waandishi wa habari na kutoa tamko
hilo ikiwa ni siku chache tangu Makonda kuvamia ofisi ya kituo cha Televisheni
chaClouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto.
“Makonda alitoa amri ya kulazimisha kurushwa hewani kwa
kipindi cha televisheni, kutumia nguvu na kupora kipindi mali ya Clouds,”
alisema Neville Meena, Katibu wa TEF.
Ilivyoanza
Februari 21, Makonda wakati akikabidhiwa eneo la ekari
1,500 lililotolewa kwa uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na kampuni ya Azimio
Estate kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo, aliulizwa swali na mwandishi wa
gazeti hili kuhusu elimu yake, badala ya kujibu alitumia simu ya mwandishi huyo
kuzungumza na Mhariri wa Habari wa JAMBO LEO na kumporomoshea matusi.
Licha ya kutoa lugha chafu, Makonda alisema habari hiyo haiwezi
kumwondoa mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji katika tuhuma
za dawa za kulevya.
Kuanzia hapo, vyombo vya habari vilifuatilia tuhuma hizo
kwa kusaka ukweli katika shule anazodaiwa kusoma huku mjadala huo ukikolezwa na
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Ilivyotokea
Siku sita baada ya Makonda kukabidhiwa eneo hilo, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alizuia ekari hizo za
ardhi kwa maelezo kuwa ni mali ya Serikali.
Akizungumza na wanahabari, Lukuvi alisema Makonda
alidanganywa kuhusu ekari hizo zilizoko eneo la Kisarawe 11 wilaya ya Kigamboni
kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Mohamed Iqbal alishindwa kesi
mahakamani ambayo ilifunguliwa na wananchi.
Kuhusu elimu, Makonda anahusishwa na mtu anayeitwa Daudi
Bashite aliyesoma shule ya msingi Koromije na sekondari ya Pamba na kumaliza
kidato cha nne kwa kupata daraja sifuri kabla ya kughushi cheti na kuendelea na
elimu ya juu.
Sakata hilo la kughushi cheti cha kidato cha nne
liliandikwa na magazeti kadhaa nchini, huku likishika kasi kwenye mitandao ya
kijamii na kila Mkuu wa Mkoa alipoulizwa, alikosa majibu.
Wakati hayo yakiendelea, Makonda anatakiwa kwenda
kujieleza katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge
akituhumiwa kukashifu wabunge kuwa wakati mwingine hukosa cha kuzungumza na ndiyo
maana husinzia bungeni.
Mjadala zaidi uliibuka baada ya Makonda kwenda Clouds
akiwa na askari wenye silaha za moto, tukio ambalo lilithibitishwa na
Mkurugenzi wa Vipindi na Uendeshaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.
Ruge alisema Makonda aliingia studio kuchukua kinguvu
sehemu ya kipindi cha Shilawadu kilichokuwa akimezuiwa kurushwa kutokana na
kutokidhi matakwa ya kitaaluma, kikimhusisha mwanamke anayedaiwa kuwa kuwa na
uhusiano na Askofu Gwajima.
Msumari
“Tunalaani vikali vitendo hivyo vya Makonda, kwa pamoja tumeazimia
kutoandika au kutangaza habari zote zinazomhusisha katika vyombo vyetu vya habari,”
alisema Meena.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanamtangaza Makonda kuwa
adui wa uhuru wa vyombo vya habari huku akibainisha atakayeshirikiana naye
kitakachompata hawatamtetea.
Meena alifafanua kuwa utekelezaji wa agizo hilo unaanza mara
moja kwani walishakubaliana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania
(UTPC) kupitia Rais wake, Deo Nsokolo.
“Kuanzia sasa mkutano na waandishi wa habari akatafute
vyombo vya habari vya nje na mwandishi wa habari atakayekwenda huko
litakalompata hakuna mtu atakayesimama kumtetea,” alisema.
“Ukienda huko ukafanyiwa jambo lolote ukatukanwa,
hatutahusika maana sisi klabu za waandishi wa habari tunajivua lawama kwa atakayekwenda
kwenye mkutano wa Makonda atakachokufanya ni juu yako.”
Alisema endapo ikitokea Makonda ameitwa bungeni, wahariri
wataamua nini la kufanya kuhusu kuripoti habari hizo.
Alisema hawawezi kuweka mipaka kwa asilimia 100 ya
kutoandika habari zake, bali kutoandika habari ambazo alikuwa akizitumia kama
ngazi na kumpa sauti.
“Kama kutakuwa na kiongozi ataambatana na Makonda kwenye
jambo lenye maslahi ya wananchi wa mkoa, waandishi watatangaza habari ya
kiongozi aliyeambatana naye na si Makonda,” alisema Meena.
Alisema waandishi wanatakiwa kushiriki matukio
anayoshiriki na si kumtangaza kwenye televisheni, redio na magazeti.
“Tungependa kutoa mwito hata kwa watu ambao wanafanya
kazi mitandaoni (online), wajue kilichowapata Clouds nao kinaweza kuwapata,”
alisisitiza.
Meena alifafanua kuwa utaratibu huo utaendelea hadi hapo
utakapotangazwa au kuamriwa vinginevyo huku akibainisha kuwa malalamiko ya
Makonda si ya leo kwani amekuwa akitoa kauli za kejeli na kudhalilisha waandishi
wa habari katika vikao vyake mbalimbali.
Alitoa wito kwa vyombo vya habari nje ya mkoa kutompa sauti
kwani kitu kitakachowakuta hakuna atakayehusika kwa lolote.
Meena alifafanua kuwa Rais John Magufuli alimwambia
Makonda achape kazi, alimaanisha si kwenda kituo cha televisheni na polisi
wenye silaha usiku.
0 comments:
Post a Comment