Abraham Ntambara
Askofu Josephat Gwajima |
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima
Josephat Gwajima amewataka waumini wake kutomjadili Rais John Magufuli kwani ni
mamlaka kutoka kwa Mungu na kuwa anaamini kiongozi huyo ameshazipata taarifa za
kuhusu mtu aliyemtaja kwa jina la Daud Albert Bashite.
Aidha, Gwajima amesema amechoka
kuzungumza na wanadamu kuhusu suala hilo na kueleza kuwa sasa anamkabidhi Mungu
ili achukue hatua ambapo yeye atafanya ibada ya kufunga na kuomba kwa siku tatu
kuanzia Machi 29 hadi 31 mwaka huu.
Alisema katika maombi hayo pia
atawaombea Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Baraza la Mawaziri, Jaji Mkuu,
Spika wa Bunge na Wabunge ili Mungu ashughulike nao.
Askofu Gwajima alisema hayo Dar es
Salaam jana, wakati wa mahubiri yake kanisani kwake Ubungo, ambapo aliwataka
waumini wake kila mmoja kumwendea Mungu kwa kufunga, kuomba na kusema kuwa
maombi hayo watajibiwa.
“Nawaambia tena, kila mtu na asikie,
sauti yangu inanyamaza, kwa habari ya kuongea na wanadamu kuanzia Jumatano, koo
langu na sauti yangu,inemwelekea Bwana wa Majeshi aliyeumba Tanzania na vyote
vilivyomo,” alisema Gwajima.
Alieleza kuwa hakuna sababu ya kulia
kana kwamba hakuna Mungu akiwataka wasiogope kwani yupo Simba wa Yuda
aliyeshinda ili pate kuifungua siri hiyo.
Aliwataka Watanzanua kutoililia mamlaka
ya Rais kwa kuwa ndiyo yanayolilinda Taifa na kulifanya litulie.
“Rais anaweza akawa sawa au asiwe sawa, lakini
hilo haiwahusu ninyi bali mumwachie
Mungu,” alisema Gwajima.
Alifafanua kwamba mamlaka ya Rais ni sawa
na mamlaka ya Mchungaji Kiongozi kama yeye ambapo alisema kuwa kama hayupo na
akawa amaharibikiwa, kanisa pia litakuwa limeharibikiwa.
Aliwataka kuachana na Rais na kuwataka
kumwendea Rais wa Mbinguni ambaye ni Yesu Kristo ambaye watamweleza haja zao, akifafanua
kuwa Rais Magufuli alisema amekwisha sikia hivyo waachane naye.
Askofu Gwajima alisema ni mwiko kanisani
kwake kusikia mtu akimsema Rais vibaya ambapo aliwataka kukaa kimya kuhusu
habari zake kwa kuwa amekwisha sikia na kwamba ni mwenye hekima, akili na
amewekwa na Mungu.
Alisema wamheshimu na kumsaidia kwa
nguvu zote Rais, lakini kuhusu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wasimsaidie na
kusema kwamba hatakubali hilo hadi haki itendeke kwani anataka kuona Tanzania
yenye usawa kwa kila Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment