*Ajikita katika kuendeleza vita vya mihadarati
*Aonya walio mabondeni wahame mara moja
Mwandishi Wetu
Paul Makonda |
HAJAKATA kiu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda kushindwa kuwajibu baadhi ya watu wanaomtuhumu kutumia
cheti cha kidato cha nne cha mtu mwingine kuendelea na elimu ya juu, hatimaye
kufika chuo kikuu.
Akizungumza jana katika hafla fupi ya kutimiza mwaka mmoja tangu
ateuliwe na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo, Makonda alijikita zaidi
kuzungumzia vita dhidi ya dawa za kulevya, mambo aliyoyatekeleza katika kipindi
hicho, matarajio yake na mikakati yake mwaka huu, bila kugusia chochote juu ya
tuhuma hizo.
Kushindwa huko kwa Makonda kumekuja takribani mwezi mmoja tangu
kuanza kwa tetesi za tuhuma hizo na gazeti hili kuziripoti kwa mara ya kwanza
Februari 22 na kisha kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii huku Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akidai kupata ushahidi wote wa Makonda
kutumia cheti cha mtu mwingine.
Makonda ambaye alitumia takribani dakika 70 kueleza masuala
mbalimbali katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa
Polisi Oysterbay na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, Makonda alisema hatishwi na
kelele zinazoendelea bila kufafanua kama ni tuhuma hizo au la.
“Sitishwi na kelele zinazoendelea…, mwaka wangu wa pili kama Mkuu
wa Mkoa nitaongeza kasi mara mbili zaidi katika vita vya dawa za kulevya,”
alisema.
Wakati akieleza hayo, taarifa zilizolifikia gazeti hili zilidai
kuwa kampuni moja kubwa itasafirisha wanahabari 10 kwenda kijiji cha Kolomije
wilayani Misungwi mkoani Mwanza, alikozaliwa Makonda, ikielezwa lengo ni kusaka
taarifa za kuzima tuhuma hizo.
Habari hizo zinaeleza kuwa safari ya timu ya wanahabari hao kutoka
vyombo mbalimbali vya habari itafanyika wiki hii ambako wameandaliwa wazee wa
kuzungumza nao kijijini hapo.
“Baadhi ya wazungumzaji ni walimu wa shule aliyosoma Makonda na
wazee wa kijiji hicho,” zilieleza habari hizo.
Licha ya kutogusia elimu yake, Makonda alitumia halfa hiyo, kutaka
wazazi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwenye vita hivyo kwa kufuatilia nyendo na
tabia za watoto wao na kutoa taarifa katika vyombo vya Dola, ili kusaidia
kutimiza ndoto na malengo yao.
“Akina mama mliobeba mimba kwa miezi sita, tunaomba mtuunge mkono
ili mateso mliyopata kwa miezi tisa, wengine mlikataliwa, wengine mlikosa hata
fedha ya kutunza mimba, wengine mlikatisha masomo yenu na wengine kupewa majina
ya hovyo, tunaomba mumuunge mkono Rais John Magufuli katika mapambano ya dawa
za kulevya,” alisema Makonda.
Alitaka wazazi kutoacha ndoto za watoto wao ambao waliwalea kwa
mateso zipotezwe na wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambapo aliwaomba
kufuatilia nyendo za watoto wao.
Aidha, alisema ana taarifa za wanafunzi kujihusisha na matumizi ya
dawa hizo akieleza kuwa wanatarajia kuendesha operesheni katika shule za mkoa
huo.
Alisema kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi kutumia dawa hizo vyooni
na kasha kuingia darasani.
Aliongeza kuwa kuna watu wamekuwa wakitumia watoto wadogo wanaotumia
dawa za kulevya katika matukio mbalimbali ya wizi na ubakaji.
Mkuu wa Mkoa alisisitiza kwa kuwaambia wazazi wasiwe wa kuamka na
kwenda kazini tu pia wawe wanafuatilia mienendo na tabia za watoto wao kwani
huwa wanavutishwa bangi, heroin na kokeni na kisha kupewa maelekezo ya kufanya
uhalifu.
Alisema wanapoona nyendo wasizozielewa waripoti Polisi ili
Serikali iwasaidie kama ambavyo imekuwa ikisaidia wengine na kufafanua kuwa
asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na dunia.
Aidha, alisema ni wajibu wa viongozi wa dini kwa mamlaka
waliyopewa na Mungu kujisikia vibaya kuwa na waumini wanaoharibika kwa kukemea
maovu hayo kwa waumini wao ambapo aliwataka kuwa mstari wa mbele kwenye vita
hivyo.
Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam, kujua kuwa vita hivyo vinatokana
na mapenzi waliyonayo kwao na kukanusha, kwamba hawafanyi kwa lengo la visasi
ambapo alifafanua kuwa ndiyo sababu ya kufanya hivyo ili kuhakikisha wananchi
wanatimiza ndoto zao.
Kwa upande mwingine, alitaka wakazi wa mabondeni kuondoka kwani
mazingira hayo ni hatarishi kwa usalama wao.
Makonda alisema atawapa viwanja wakazi wote wenye hati wanaoishi maeneo
hayo hatarishi na kwamba pamoja na kuwapa viwanja, Serikali ya mkoa
itashughulikia watumishi waliotoa hati hizo huku wakijua maeneo hayo hayaruhusu
makazi ya watu.
0 comments:
Post a Comment