Hussein Ndubikile
JUMUIYA ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Afrika (SADC) imehamasisha raia wao wenye taaluma na wasionazo kujisajili
ili kupata fursa za kujiunga na Jeshi la Ulinzi wa Amani la Jumuiya hiyo.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na
Msajili na Mkufunzi wa SADC, Eliet
Magogo, katika warsha ya mafunzo ya kuhamasisha raia kujisajili na Jeshi hilo.
Alisema kutokana na mwamko mdogo wa raia
wa nchi za SADC kujisajili, Jumuiya imeanza mafunzo kwa maofisa wa taasisi za Serikali
lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watakaojiunga.
"SADC inaendesha warsha kwenye nchi
wanachama na usajili ukienda vizuri itapata watu wengi watakaohudumia Jeshi
hili," alisema Magogo.
Alisema waombaji wenye taaluma
watatakiwa kuwa na elimu ya Shahada na uzoefu wa miaka saba ya taaluma yao,
huku akiongeza kuwa suala hilo halizuii raia wa kawaida kujisalili kwani ndani
ya Jeshi hilo kuna wigo mpana wa majukumu.
Aliongeza kuwa waombaji watafanyiwa
mchujo kwa kufuata vigezo vilivyowekwa na watakaofanikiwa kuchaguliwa
watapelekwa Chuo cha Mafunzo nchini Zimbabwe.
Alisisitiza kuwa katika Jeshi hilo watu
wenye taaluma za udaktari, uhasibu, ukaguzi wa hesabu, uhandisi, uanadiplomasia
na wa mawasiliano ya umma wanahitajika.
Alifafanua kuwa kwa wanaotaka kujiunga
na Jeshi hilo waingie kwenye mtandao wa SADC ili kupata maelekezo na vigezo
vinavyotakiwa.
Pia alisema raia watakaochaguliwa na
kupewa mafunzo wataitwa kujiunga na Jeshi endapo watahitajika na kupelekwa nchi
zitakazokuwa na matatizo ya usalama.
0 comments:
Post a Comment