Abraham Ntambara
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli kuendeleza
Mchakato wa Katiba Mpya kwa kuanzia ilipoishia Rasimu ya Pili ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa ACT,
Msafiri Mtemelwa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
Alimtaka Rais Magufuli kuendeleza mchakato huo hadi Katiba hiyo
mpya itakapokamilika. “Rais Magufuli aanze na Rasimu ya Jaji Warioba iliyokuwa inatoa
nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotekeleza wajibu wao kulingana
na nafasi walizonazo,” alisema Mtemelwa.
Alisema kwa namna wanavyomfahamu Rais Magufuli ambaye amekuwa
akijinasibu kuwa Rais wa wanyonge, wanaamini hatalinda maslahi ya chama chake
CCM pekee, bali atawapatia Watanzania Katiba bora kwa maslahi ya Taifa.
Kwa mujibu wa Mtemelwa, Katiba bora itamnufaisha kila Mtanzania na
akawaomba viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kulitilia mkazo suala hilo ili
Katiba Mpya yenye kukidhi kiu na matakwa ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu mkuu huyo wa ACT alisema chama
hicho jana kilianza kutoa fomu kwa wanachama wanaohitaji kugombea nafasi ya
kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na kuwataka
wanachama wenye sifa wajitokeze.
Alieleza kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo ndani
ya chama utakamilika Machi 21 mwaka huu saa 10:00 jioni ambapo alisema kwa
wanachama wa Dar es Salaam watachukua fomu hizo Mako Makuu ya ACT huku walio
mikoani wanatakiwa kuwasiliana na Afisa Mawasiliano.
Alisema maandalizi ya mkutano mkuu wa kidemokrasia wa ACT yamekamilika
kwa zaidi ya asilimia tisini ambapo watakuwa na mijadala mbalimbali kutoka kwa
wawakilishi wa taasisi za ndani na nje.
Alisema mkutano huo utawashirikisha wanachama na wasio wanachama
huku ukiwa hauna wajumbe Mahususi ambapo utajikita zaidi katika masuala ya
maendeleo ya nchi na dunia kwa jumla.
0 comments:
Post a Comment