Suleiman Msuya
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema hakina
muda wa kujibizana na Profesa Ibrahim Lipumba, kwa madai kuwa kundi analoongoza
ni la wahuni.
Aidha, CUF imesema hakuna kikao chenye
mamlaka ya kumfukuza au kumwondoa madarakani Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad tofauti na mkutano mkuu wa chama hicho.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati
ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro wakati akizungumza na JAMBOLEO jana, ikiwa ni
siku chache baada ya Lipumba kutangaza kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Chama
hicho, limekubaliana kumkaimisha Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya nafasi ya
Seif.
Alisema wao chama hawana muda wa kukaa
na kujadili uamuzi wa kundi la watu ambao alidai ni wahuni hivyo bado wanatambua
kuwa Maalim Seif ndiye Katibu Mkuu wao.
Mtatiro alisema Lipumba na kundi lake
walishafukuzwa CUF hivyo wanachokifanya kwa sasa hakina tija kwa chama wala kwa
wanachama wao.
Mwenyekiti huyo alisema ni aibu
kutangaza kuwa Baraza lilikaa na kumteua Sakaya kuwa Katibu wakati hakuna
mabaraza mawili ndani ya chama hicho.
“Wakati mwingine ukimwangalia Lipumba na
kundi lake, anaonekana amechanganyiwa kinachomlinda ni nguvu ya Dola kumlinda
kwani sisi tunawaona ni wahuni fulani ambao wanapingana na ukweli,” alisema.
Mtatiro alitoa mwito kwa wanachama wa
CUF kuendelea kushikamana na kuachana na propaganda za Lipumba na kundi lake,
kwani hazina nia njema katika chama.
“Sisi hatumtambui Lipumba kama kiongozi
wala mwanachama wa chama chetu, hivyo lolote ambalo linafanyika kupitia wao hatuna
kazi nalo ni kupoteza muda,” alisema.
Kuhusu mgombea wa Bunge la Afrika
Mashariki (EALA), alisema wao wametekeleza agizo la Bunge na kupeleka mgombea
mmoja, hivyo iwapo hao wa Lipumba watapitishwa si jukumu lao.
0 comments:
Post a Comment