*Mwigulu aweka wazi
kuwa si askari Polisi
*Awataka makamanda
wawashauri viongozi
Sharifa Marira, Dodoma
Mwigulu Nchemba |
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema
mtu aliyemshikia bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye amekamatwa na si askari Polisi.
Mwigulu alisema hayo jana kwenye mahojiano na waandishi
wa habari baada ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Waandamizi wa Polisi na
Makamanda wa Mikoa na Vikosi.
"Kama nilivyokuwa nimeagiza uchunguzi ufanyike
kumbaini mtu aliyemshikia Nape bastola hadharani ni kwamba si askari Polisi na amekamatwa,
hivyo taratibu za kuwajibishwa zitaendelea huko kwenye Mamlaka husika," alisema
Mwigulu bila kufafanua ni Mamlaka ipi.
Hata hivyo, Mwigulu aliulizwa kama mtu huyo ni raia wa
kawaida au ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kama inavyoarifiwa na baadhi ya mitandao
ya kijamii, lakini alikataa kufafanua suala hilo.
Wiki jana, Nape alinyooshewa bunduki na mtu huyo wakati
akishuka kwenye gari lake karibu na hoteli ya Protea, Oysterbay, Dar es Salaam
alipokwenda kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kutumbuliwa kwake.
Awali kwenye mkutano huo, Mwigulu alitaka maaskari
kufanya kazi yao kwa weledi na kutenda haki kwani katika ziara alizofanya mikoani
kwa nyakati tofauti, alilalamikiwa na wananchi kubambikiwa na kubadilishiwa
kesi, jambo ambalo linakiuka misingi ya kazi za kipolisi.
"Kuna malalamiko juu ya askari kubambika na
kuwabadilishia watu kesi, hili haliko sawa tuwape watu haki zao, sisi tupo kwa
ajili ya wanaoonewa hata Rais wetu anasisitiza kuwa Serikali yake ni ya
wanyonge na tufanye kazi kwa haki," alisema Mwigulu.
Alitaka polisi kutotumia taarifa za mahasimu peke yao kuhukumu,
kwani kumekuwa na tabia ya kutengenezeana kesi hali inayofanya wakosefu kubaki
uraiani na wasio na hatia kufungwa.
Mwigulu pia alisema polisi wataendelea kushirikiana na taasisi
zinazohusika na dawa za kulevya ili kupambana na vita hivyo ambavyo vimeanza
nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama, Balozi Adadi Rajabu, alishauri makamanda wa Polisi wa mikoa kueleza viongozi
wao wa mikoa wanapotaka kufanya jambo linalokwenda kinyume na haki na taratibu
za nchi wasifanye hivyo.
"Makamanda wa mikoa tumieni nafasi mliyonayo kuonya
viongozi wenu wa mikoa, mnapoona wanataka kuanzisha jambo ambalo linakwenda
kinyume, msisubiri waharibu ndipo mseme, mkiacha jambo likishatokea ni vigumu
kulifuta na kuleta picha mbaya kwa jamii," alisema Adadi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest
Mangu, alisema sifa ya polisi ni nidhamu na kwamba hawatavumilia maaskari watakaokwenda
kinyume na maadili.
Alisema katika suala la utendaji, Jeshi hilo litaendelea kuendesha
operesheni zikiwamo za kupambana na dawa za kulevya ambapo hadi sasa wameteketeza
mashamba kadhaa ya bangi na mirungi, kupambana na ujangili, biashara za magendo
kutoka nje na ucheleweshaji na ubambikaji kesi.
0 comments:
Post a Comment