Suleiman Msuya
Kassim Majaliwa |
IKIWA takribani miezi mitatu baada ya
kuibuka kwa sakata la kupotea faru aliyebatizwa jina la John, Tume ya Uchunguzi
iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, imethibitisha kuwa faru huyo alikufa.
Aidha, Tume hiyo imependekeza kwa Serikali
kuwachukulia hatua waliohusika kumhamisha faru John bila kufuata utaratibu hali
ambayo ilisababisha kifo chake.
Akiwasilisha matokeo ya Tume hiyo ya
uchunguzi, Mwenyekiti wake, Profesa Samwel Manyele ambaye ni Mkemia Mkuu wa
Serikali alithibitisha kuwa John amekufa, baada ya sampuli 45 kuthibitisha bila
shaka.
Alisema kupitia wataalamu walioshiriki kazi
hiyo, Afrika Kusini matokeo yanaonesha sampuli na vielelezo vyote ni vya mnyama
huyo.
“Mzoga, fuvu, pembe (zote tatu) damu,
zote ni za Faru John, zilichukuliwa wakati wa kumwekea kifaa maalumu cha kutambua
aliko,” alisema.
Alisema jumla ya sampuli za vielelezo 45
zilitumika na kuonesha kuwa ni Faru John ambaye alikuwa dume mweusi, hata pembe
ambazo ziliwasilishwa kwa Waziri Mkuu ni za kwake.
Alisema faru huyo alifia Sasakwa Grumeti
ambapo alikuwa amehifadhiwa, huku kukiwa na upungufu mwingi uliotajwa kusababisha
kifo chake.
Sababu
Mwenyekiti huyo ambaye alisema John
alikufa kutokana na kukosa matunzo, uangalizi wa karibu na matibabu alipougua, pia
kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria ukiwamo upungufu wa kiuongozi kwa wizara,
hifadhi hata taasisi zake.
Alisema katika uchunguzi wao, walibaini
upungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja kukosekana kibali rasmi cha kumhamisha John
pamoja na kuonesha kuwa mchakato uliridhiwa na Wizara.
“Hapakuwa na kibali rasmi kutoka kwa
Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwenda Grumeti,” alisema.
Alisema Tume inashauri taratibu za
kuhamisha wanyama walio katika hatari ya kutoweka ziwe bayana, ziainishwe
kwenye kanuni na sheria, kwani hakuna kiongozi au mtaalamu aliyeona umuhimu wa
kibali.
“Tume ililitazama sula hili kwa jicho lingine.
Kama mbuzi na ng’ombe wanasafirishwa kwa vibali mikoani kote, iweje faru huyo
asafirishwe bila kibali,” alisema.
Alisema kutokana na upungufu wa
kiutendaji uliofanywa na ofisi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini na Mhifadhi
wa NCAA na kuruhusu Faru John kuondolewa bila kibali, Tume inashauri hatua za
kiutawala zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Manyele alisema migongano ya kimaslahi
kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wenye kusimamia maslahi
binafsi ni sababu nyingine ya faru huyo kuhamishwa.
“Maslahi binafsi hadi kufikia ngazi ya
wizara, ambako wizara iliingilia kati na kupendelea upande wenye maslahi
binafsi, hali hiyo ilisababisha kutoelewana kwa makundi hayo mawili, hadi
kufikia hatua ya kushitakiana kwa kutumia kauli ya kuuzwa kwa Faru John,”
alisema.
Alisema Tume inashauri Serikali iunde tume
huru kuchunguza migogoro ya kimaslahi kati ya watumishi wa NCAA dhidi ya
uwekezaji ndani ya hifadhi na hatua stahiki zichukuliwe.
Mkemia Mkuu alisema upungufu wa
kiuongozi katika kushughulikia masuala ya watumishi ni mwingi hata baada ya
mtumishi Lemanya kuwasilisha malalamiko yake kwa uongozi wa NCAA ya kudaiwa
kupokea Sh milioni 50 baada ya kumhamishwa faru huyo, malalamiko yake
hayakushughulikiwa na uongozi.
“Tume inaunganisha (2) na (3) na
kushauri Serikali ifanye tathmini ya kina kuona kama uongozi uliopo sasa NCAA
unatosha kuendelea kuongoza taasisi hiyo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Aidha, alisema uwepo wa taasisi nyingi
zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori mipaka yao ya
kiutendaji inakuwa vigumu kujulikana.
Alisema Tume inashauri sheria husika
zipitiwe upya na kubainisha majukumu mahsusi ya kila taasisi, pia uwezekano wa
kujumuisha mamlaka hizo.
Ushauri
Alisema Tume inashauri kufanyika
utambuzi wa wakazi halali ndani ya bonde la Ngorongoro na maeneo mengine ya
Serengeti na kuzuia uhamiaji katika maeneo hayo.
Pia inashauri kuanzisha na kuimarisha maabara
ya utambuzi wa vinasaba vya wanyamapori chini ya GCLA ili kutoa msukumo kwa
vyombo vya haki jinai katika kupeleleza na kuchunguza kazi zinazohusu ujangili.
Halikadhalika alisema Tume inaomba
Serikali iimarishe vikosi vya kuzuia ujangili kwa kushirikisha na Jeshi la
Wananchi, kwa namna inavyoonekana itafaa.
“Mwingiliano
kati ya mifugo na wanyamapori unatoa mwanya kwa majangili kutumia nafasi hiyo
kufanya uhalifu. Tume inashauri pia kuwapo
udhibiti na sheria kali ya kuzuia mifugo katika maeneo ya hifadhi,” alisema.
Pia alisema vibali vya uwindaji wanyama
wanaoelekea kutowekwa (faru na tembo) vifutwe na sheria ipitiwe upya ili kuzuia
vibali hivyo.
Alisema viwanja wa ndege ndani ya
hifadhi, vifanyiwe tathmini ya kina juu ya manufaa ya uwepo wao, usimamizi na
uendeshaji wao ili kulinda maslahi ya Taifa.
Profesa Manyele alisema Tume inashauri
kuanzishwa kwa kanzidata ya vinasaba vya wanyamapori ambayo itasaidia kutambua
nyara na kuwezesha vyombo vya uchunguzi na upelelezi kukamilisha kazi zao.
Alisema mahojiano yalishirikisha watendaji
18 ambapo mchakato mzima ulionesha kwa asilimia 100 kuwa Faru John amekufa.
Majaliwa
Akizungumza baada ya kupokea ripoti
hiyo, Waziri Mkuu alisema ataipitia ripoti hiyo ili kuilewa na kama kutakuwa na
hatua za kuchukua Serikali itafanya hivyo.
Majaliwa alisema walilazimika kuunda
tume hiyo kutokana na matukio mbalimbali ya ujangili, hivyo kupitia ripoti hiyo
watakuwa na pa kuanzia.
“Nitaipitia ripoti hii kwa umakini kwani
kifo cha Faru John kiliibua maswali mengi, naamini utakuwa mwanzo mzuri kwa
Serikali kukabiliana na janga hili la ujangili,” alisema.
Aidha, alisema gharama ambazo zimetumika
kwa tume hiyo zitabainishwa baadaye, baada ya kila taasisi kuwasilisha gharama
iliyotumika kwa watumishi wake.
Aidha,
Tume iliilalamikia Wizara ya Maliasili na Utalii kuvujisha siri za ndani kati
ya wizara na taasisi zingine jambo ambalo si sawa.
“Katika kutekeleza jukumu hili zito,
Tume ilishuhudia kuvuja kwa siri za mawasiliano kati ya Mkemia Mkuu wa Serikali
na Wizara juu ya vibali na usafirishaji wa sampuli kwenye magazeti,” alisema.
0 comments:
Post a Comment