Suleiman Msuya
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema amri ya Rais
John Magufuli kuzuia mchanga wa dhahabu kutoka katika migodi mbalimbali
kusafirishwa kwenda nje umelipotezea Taifa Sh. trilioni 1.8 ambazo zingelipwa
kama kodi ya ongezeko la mtaji.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo alisema
hayo mkoani Arusha katika kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la
Arusha juzi.
Alisema ni jukumu la viongozi kuzingatia umakini katika utoaji
kauli mbalimbali ili kuepusha migongano au hasara kwa Taifa.
“Juzi katika mkutano wetu pamoja na kuzungumzia Azimio la
Arusha nilizungumzia suala la umakini wa viongozi katika kauli zao kiongozi
lazima ujue unatoa kauli gani wakati gani,” alisema.
Kupitia waraka alioutuma kwa vyombo vya habari, Zitto alisema
aliwaeleza wanachama na wageni wengine katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa amri
aliyoitoa Rais Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu imesababisha
Taifa kupoteza dola za Marekani milioni 880.
Alifafanua kwamba fedha hizo zingelipwa kama kodi ya
ongezeko la mtaji kutokana na mauzo ya Kampuni ya Madini ya Acacia
yaliyokwishaanza lakini yamevunjika baada ya amri ya Rais Magufuli.
Kiongozi huyo alisema hivi sasa Tanzania ina sheria ya
kutoza asilimia 20 ya thamani ya mauzo iwapo kampuni zinauziana hisa.
Alisema sheria hiyo ilitungwa mwaka 2012 ili kukabili
wawekezaji waliokuwa wanauziana kampuni bila Tanzania kupata lolote.
“Tanzania imeshafaidika na kodi hiyo kwa mauzo mbalimbali
ambayo yamekwisha fanyika kwenye sekta mbalimbali,” alisema.
Mbunge huyo alisema wakati Rais anatoa amri kuzuia mchanga wa madini kusafirishwa nje ya nchi,
kulikuwa na mazungumzo yakiendelea kati ya Kampuni ya Acacia ( yenye migodi inayozalisha nchini Tanzania ambazo
- Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyengine ya nchini Canada ambapo
ingenunuliwa kwa dola za Marekani bilioni 4.4 .
Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema tafiti zinaonyesha
kuwa gharama ya kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu nchini ni dola za Marekani
milioni 800 hivyo mapato ambayo yangepatikana kutokana na kodi ya mauzo ya
Acacia yangewezesha nchi kujenga kiwanda hicho na kufikia lengo la Rais la kuwezesha
uchenjuaji wa mchanga hapa hapa nchini.
“Rais angetulia, angeweza kuua ndege wawili kwa jiwe
moja, kiwanda cha kuchenjua kingejengwa nchini na mchanga usingesafirishwa tena
kwenda China na Japan,” alisema Zitto.
Alibainisha kuwa Tanzania haina mchanga wa kutosha wa
kushibisha mtambo wa uchenjuaji madini kwa mujibu wa teknolojia ya sasa.
Alisema fedha hizo zingiweza kutumika katika miradi ya
maendeleo mbalimbali kama ujenzi wa reli ya kisasa ambapo Serikali imeshaingia
mikataba na kampuni mbalimbali hivyo kuepuka kukopa.
Aidha, alisema pia fedha hizo zingesaidia ujenzi wa vyuo
vya veta kila wilaya na kila kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na chenji
ingebaki.
“Tanzania inahitaji Sh. bilioni 750 kujenga vyuo vya Veta
kila wilaya, miji, manispaa na majiji yote nchini,” alisema.
Alisema: “Binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue
dhahabu hapa hapa nchini badala ya kupeleka mchanga Japan na China lakini ni
muhimu uamuzi huo uwe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko yenye madhara.”
0 comments:
Post a Comment