Mwandishi Wetu
Theophil Makunga |
BODI ya Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF) imesisitiza vyombo vya habari kuendelea na msimamo wa kutoandika habari
zozote ambazo kumhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa
Bodi hiyo, Theophil Makunga baada ya kikao kilichofanyika Dar es Salaam ambapo wajumbe
walisisitiza msimamo huo hadi Makonda atakapotambua kosa lake na kuomba radhi.
Alisema TEF ilijadili mwenendo wa vyombo
vya habari ndani ya wiki moja tangu ilipotoa msimamo wa kutotangaza habari za Mkuu
huyo ambapo hadi jana waliona kuwapo mshikamano.
“Bodi ilipitia habari za Mkuu wa Mkoa
zilizochapishwa tangu ulipotolewa msimamo wa kumfungia kuwa zinaridhisha hivyo
tunawaasa wahariri na wanahabari kuendelea hivyo hivyo,” alisema.
Bodi iliwapongeza wahariri waliotekeleza
kwa usahihi msimamo wa kutochapisha habari za Mkuu wa Mkoa kwa wiki hiyo nzima.
Aidha, alisema Bodi iliwataka viongozi
wa mitandao ya kijamii kuunga mkono msimamo huo ili kuwa fundisho kwa kiongozi
huyo.
Makunga alisema Makonda amewekewa
vikwazo maalumu kwa mikutano atakayoandaa au matukio atakayoongoza habari zake hazichapishwi.
Alisema Bodi ilikipongeza kituo cha
Clouds Media kwa kumsimamisha kazi mtangazaji aliyekiuka msimamo huo.
Aidha, alisema Bodi pia iliwasiliana na
uongozi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kukubaliana
kwamba msimamo huu uendelee.
TEF na UTPC kwa pamoja walitoa tamko la
kutoandika habari yoyote ya Makonda baada ya kuvamia Clouds Media akiwa na
askari wenye silaha usiku jambo ambalo halikubaliki katika nchi zinazosimamia
misingi ya sheria na utawala bora.
0 comments:
Post a Comment