Waandishi Wetu
Makonda akihojiwa na Kamati ya Bunge |
HATIMAYE. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhojiwa kwa dakika 180 na kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na kauli aliyoitoa Februari mwaka huu inayodaiwa kudhalilisha
hadhi ya mhimili huo wa Dola.
Makonda akiwa amevaa shati ya maua na suruali nyeusi
aliwasili bungeni jana saa 4 asubuhi kuitikia wito huo uliopitishwa na Bunge Februari 8
mwaka huu, ikiwa zimebaki siku saba tu kabla ya kuanza vikao vya Bunge la
Bajeti.
Siku hiyo ya Februari 8, Bunge lilitumia dakika 45
kupitisha kwa kauli moja maazimio manne, likiwemo la kuitwa kwa Makonda na mkuu
wa wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kutokana na hoja iliyowasilishwa na
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara akisema wateule hao wa Rais wametoa kauli
zinazodhalilisha Bunge.
Wakati Makonda akisema wakati mwingine wabunge hulala
bungeni kwa kukosa cha kuzungumza, Mnyeti aliandika katika ukurasa wake wa
facebook kuwa wabunge ni wapuuzi kutokana na michango yao wakati walipohoji
hatua ya Ma-DC na Ma-RC kutoa amri za kuwaweka ndani viongozi wa siasa.
Hata hivyo, jana
ilikuwa zamu ya mkuu huyo wa mkoa ambaye habari za ndani kutoka katika kamati
hiyo zinaeleza kuwa alikiomba radhi chombo hicho cha kutunga sharia, baada ya
kubanwa kwa maswali ambayo mengine alishindwa kuyajibu.
Kuhojiwa kwa mteule huyo wa Rais, huenda kukawatuliza
baadhi ya wabunge walionukuliwa katika vyombo mbalimbali vya habari wakieleza
kuwa iwapo Bunge lingeshindwa kumhoji mkuu huyo wa mkoa, moto ungewaka katika
vikao vya Bunge la bajeti.
Hata hivyo, mteule huyo wa Rais bado anaweza kuzua gumzo
bungeni kutokana na kauli na matukio mbalimbali yanayomhusu, likiwamo la
kuvamia kituo cha Clouds ambalo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Nape Mnauye aliliundia tume iliyothibitisha Makonda kuvamia kituo
hicho, ambayo hata hivyo yanatajwa kusababisha Nape kuvuliwa uwaziri.
Jingine ni utata wa elimu ya Makonda na madai ya kughushi
na kutumia vyeti vya kidato cha nne vya mtu mwingine, ambayo mashtaka yake
yamefikishwa Tume ya Maadili ya Viongozi na Meya wa Manispaa ya Ubungo,
Boniface Jacob.
Akizungumza baada mahojiano hayo, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, George Mkuchika alisema, “Leo (jana) tumekutana baada ya kuagizwa na
Spika kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Kamati yetu hukutana pale tu inapoagizwa na Spika.”
“Spika aliagiza kamati yetu imuite makonda ili kumhoji
kufuatia azimio la Bunge lililopitishwa Februari 8. Pamoja ana mambo mengine
alitakiwa kufka mbele ya kamati kujibu tuhuma zinazomkabili.”
Mkuchika alisema kwa mujibu wa azimio hilo, Makonda alidaiwa
kutoa kauli hiyo kupitia kituo cha Televisheni cha Clouds kwamba wabunge
wanasinzia, jambo alilosema kuwa lilionekana kama dharau kwa Bunge.
“Napenda kutoa taarifa kuwa Makonda leo (jana) amekuja
mbele ya kamati na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na naweza
kusema kuwa kamati imemaliza kazi yake iliyoagizwa,” alisema Mkuchika.
Alisema kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chombo hicho
cha kutunga sheria, kamati yake itakabidhi taarifa ya mahojiano hayo kwa Spika
ambaye ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu kazi ya kamati hiyo.
Maazimio ya Bunge yalivyoshangaza
Ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge kwa
azimio la aina hiyo kupitishwa bila kusikika sauti ya “siyooo” licha ya kwamba
ndani ya Bunge, walikuwamo mawaziri kadhaa na wabunge wa chama tawala cha CCM.
Mjadala huo uliibuliwa na Waitara kupitia kanuni ya 51
katika tukio ambalo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alipata
upinzani mkali kutoka kwa wabunge alipojaribu kulisihi Bunge lisipitisha azimio
la kuwajibishwa kwa wateule hao kabla hawajasikilizwa.
Miongoni mwa maazimio manne yaliyopitishwa ni pamoja na
linalotaka wateule hao wa Rais wachukuliwe hatua za kisheria kama itabainika
walitenda makosa yanayoangukia kwenye jinai.
Bunge pia liliazimia kuwa endapo kamati itaridhika kwamba
kuna jinai, AG awasiliane na vyombo vingine vya kiuchunguzi kufuatilia suala
hilo na kuchukua hatua kwa taratibu za vyombo hivyo.
Vilevile, Bunge liliazimia kwa kauli moja kuwa Waziri wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), atume waraka kwa wakuu wa
mikoa na wilaya kutoingilia mhimili wa Bunge.
Katika azimio jingine, endapo kamati hiyo ya Bunge
itathibitisha tuhuma dhidi yao, Bunge linaazimia mamlaka ya uteuzi ijulishwe
ili kuwawajibisha.
0 comments:
Post a Comment