Salha Mohamed
TAASISI ya
Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya upasuaji wa kihistoria kwa wagonjwa
kuwekwa mishipa sita ya damu iliyoziba kwenye moyo baada ya kuivuna kutoka
miguuni.
Upasuaji huo
ulifanyika kwa kushirikiana na madaktari kutoka hospitali ya Saifee nchini
India ikiwa ni ahadi ya kiongozi wa Mabohora kwa Rais John Magufuli.
Daktari Bingwa
wa Upasuaji wa Magojwa ya Moyo na Mishipa ya Damu JKCI, Dk Bashir Nyangasa
alisema upasuaji huo umeokoa Sh milioni 400 endapo wangesafirishwa nje ya nchi.
Alisema
wamefanya upasuaji kwa wagonjwa 20 ambapo kati yao 12 walifanyiwa upasuaji bila
kufungua vifua, ambapo walizibua mishipa ya damu iliyokuwa imeziba huku mmoja
ukiwa uliziba kwa asilimia 100.
"Tumefanyia
wagonjwa wanne kwa kuvuna mishipa kwenye miguu na kuipandikiza kwenye moyo,
namshukuru Mungu katika uhusiano na watu wa nje kila wanavyokuja hufanya lililo
bora zaidi," alisema.
Alisema kambi
zilizopita walikuwa wanavuna mishipa ya damu miguuni na kuiweka kwenye moyo kwa
mishipa miwili au mitatu, lakini kwa ushirikiano huo walifanyia mishipa sita.
"Mishipa
sita ni historia kufanyika nchini, mishipa hiyo iliyowekwa mgonjwa, kuunganisha
kila mshipa huchukua dakika sita hadi nane lakini hawa walifanya kwa dakika nne
hadi tano," alisema.
Alisema walitanua
milango ya moyo ambayo ilikuwa haipitishi damu vema, walibaini pia matatizo
katika mishipa ya damu ya moyo na kuweka betri kwa mgonjwa.
Alifafanua: “Kuna
wagonjwa wawili ambao matundu yao ya moyo yalikuwa yameziba na walipewa
matibabu na wanaendelea vizuri pamoja na mtoto wa miaka minane ambaye valvu
yake ya moyo ilikuwa imesinyaa”.
Mkurugezi wa
Tiba ya Moyo, Dk Peter Kisenga alisema kupitia ushirikiano huo, walijifunza
mambo mbalimbali kutoka kwa madaktari hao wa India katika upasuaji, hasa bila
kufungua vifua na kuzibua mishipa iliyoziba kabisa.
Aidha,
miongoni mwa madaktari kutoka hospitali ya Saifee, Yunus Loya alishukuru kwa
mapokezi mazuri waliyopata na walibadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji.
Makamu
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora nchini, Zainuddin Adamjee alisema wataendelea
kushirikiana na Tanzania kutoa huduma za kijamii na kwamba Februari walileta
madaktari wengine kufanya kazi Arusha.
0 comments:
Post a Comment