Suleiman Msuya
Constatine Akitanda |
MWENYEKITI wa Chama Cha Kijamii (CCK),
Constatine Akitanda, amesema iwapo hakutakuwa na hatua zitakazochukuliwa kuhusu
kauli na uendeshaji wa nchi, Taifa litakwama.
Akitanda alisema hayo jana wakati
akizungumza na JAMBOLEO Dar es Salaam akibainisha kuwa kila mtu ameweka kichwa
chini na kushindwa kutoa ushauri kwa watawala.
Alisema iwapo nchi itaendeshwa bila ushauriano,
kusikilizana na kuchukuliana hatua, ni dhahiri nchi inaweza kukwama kwa siku za
karibuni.
Mwenyekiti huyo alisema kauli za
kiongozi wa nchi kuwa hakuna mtu aliyemchukulia fomu ya kugombea urais, anaamini
haina afya kwa jamii hata Taifa la Tanzania.
Alisema ni vema Katiba, sheria na kanuni
za uongozi zikazingatiwa ili kulinusuru Taifa na iwapo kikombe cha uovu kikijaa
ni vigumu nchi kutawalika.
“Nchi hii ina watu wenye akili wanaopaswa
kusikilizwa, lakini kwa sababu hatusikilizwi ndiyo maana tumenyamaza ila
tunafuatilia kila jambo,” alisema.
Akitanda alisema Tanzania ni ya
Watanzania wote, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kusikilizwa na isionekane
kuwa mtu mmoja au kundi fulani ndilo litavusha nchi.
Alisema kila kona ya nchi Watanzania
wanalia kutokana na aina ya utawala ambao alidai kuwa una vimelea vya ubabe
jambo ambalo si sahihi.
Mwenyekiti huyo alisema CCK inatafakari
na kukusanya kila jambo ambalo linaendelea, ili kujiridhisha na wakati ukifika
watatoa taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo.
Alitoa mwito kwa umma kuendelea
kuvumilia na kuipigania Tanzania yao, ili kufanikisha dhamira ya maendeleo
ambayo imekuwa ikiimbwa na Rais John Magufuli.
Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahim Dovutwa
alisema ili kuifanya nchi iendeshwe kwa misingi ya kidemokrasia ni vema Katiba
ya mwaka 1977 iangaliwe upya kwa maslahi ya Taifa.
“Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 37
inasema Rais halazimishwi kupokea ushauri wa mtu yeyote, hivyo ni lazima Katiba
iangaliwe upya kwani inampa madaraka makubwa Rais,” alisema.
Dovutwa alisema mikakati yao ni
kuhakikisha Katiba inatambua mgombea binafsi, uhuru wa tume ya uchaguzi, rais
apingwe mahakamani, mahitaji ya kisheria ya vyama vya siasa na rais apate zaidi
ya asilimia 50 ya kura.
Alisema watu wamesahau katika tawala
zote zilizopita changamoto ni lazima ziwepo kutokana na upya wa uongozi na malengo
ambayo kiongozi amejiwekea.
“Mwinyi (Rais Ali Hassan), Mkapa (Rais
Benjamin) na Kikwete (Rais Jakaya) walikutana na changamoto hizo katika awamu
zao za kwanza hivyo ni vema wananchi wakazoea ila baadaye watafaidika,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment