Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema
Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao wanapewa kazi lakini
wanashindwa kuzimaliza kwa muda uliopangwa.
Atoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza
na watumishi wa Halmashauri ya Chalinze na wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa
Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la Mto Wami, Bagamoyo
mkoani Pwani.
Alikwenda kukagua mradi wa upanuzi wa
mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza majisafi
na matangi ya kuhifadhi maji ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika.
Awamu ya kwanza ilianza Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.
Alimwagiza Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Gerson Lwenge ahakikishe ujenzi wa mradi huo unafikia asilimia 80
la sivyo, wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi
mwingine.
Agizo la Waziri Mkuu linatokana na
taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo, Overseas Infrastructure
Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India, alipaswa kumaliza kazi hiyo Februari 22 lakini
hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 23 tu.
“Nimeelezwa kwamba mmempa nyongeza ya
siku 100 ambayo inakwisha Mei 31, kama kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na
kufikia angalau asilimia 80, itabidi Waziri uendelee na taratibu zako za
kukatisha mkataba, tuanze kutafuta mkandarasi mwingine,” alisema.
“Hii kampuni niliikuta Lindi kwenye
mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa maagizo ya kuharakisha ujenzi
ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi Rais alipokwenda na kuagiza mkandarasi
anyang’anywe pasipoti yake ya kusafiria mpaka atakapomalizia kazi.
“Kwa kifupi hii kampuni haina uwezo wa
kufanya hizi kazi, na ndiyo maana hadi sasa wamekamilisha asilimia 23 tu ya
mradi wakati walipaswa kuwa wamemaliza hivi sasa,” alisema Waziri Mkuu na
kuongeza:
“Waziri endelea na utaratibu wa
kuwaondoa kisheria kwa sababu hata tukiwaongeza muda bado hawatakamilisha kazi.
“Nimesikitika sana kukuta mkandarasi
hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe na uwezo wa kifedha wa
kuifanya ile kazi ili hata Serikali ikichelewesha malipo yake, yeye aendelee na
kazi,” aliongeza Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu ufanisi wa mradi
huo, Waziri Mkuu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa CHALIWASA, Christer Mchomba,
ahakikishe anapeleka maji hadi majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi
walipe bili zao badala kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vibanda.
“Kazi
ya kupeleka maji majumbani ni yenu CHALIWASA na si ya Wizara. Pelekeni maji na
mfunge mita ili watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia toeni elimu kwa wananchi
kupitia mikutano ya hadhara, waelezeni mipango yenu na wapi mlipofika. Kazi
yenu si kutandika mabomba tu, bali kutekeleza majukumu mliyopewa kwa niaba ya
Serikali,” alisema.
Kuhusu mitambo inayotumika, Waziri Mkuu
alisema mashine zilizopo ni za siku nyingi tangu mwaka 2003; hivyo alimwagiza
Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji mashine za kisasa kwani hilo suala ni kubwa
na haliwezi kubebwa na CHALIWASA.
“Bora mngeanza kuagiza mashine mpya hivi
sasa, badala ya kusubiri zichakae kabisa, ndipo muanze kufikiria kuagiza,”
alisema.
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo,
Mchomba alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi huo ilisainiwa Mei 18 mwaka
juzi kati ya DAWASA na OIA yenye ubia na kampuni ya Pratibha Industries kutoka
India kwa dola milioni 41.36 ambazo ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya
Exim ya India.
“Kazi zilizopangwa kufanyika ni upanuzi
wa mtambo wa maji ili kuongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa
siku; ujenzi wa mfumo wa mabomba ya kusambaza maji wenye kilometa 1,022; ujenzi
wa matangi makubwa 19 ya kuhifadhia maji; vituo tisa vya kusukumia maji na vibanda
351 vya kuchotea maji,” alisema.
Alisema
hadi sasa mkandarasi huyo ameshalipwa dola milioni 15.81 sawa na asilimia 38 na
anaendelea na utandazaji mabomba ambapo hadi sasa ameshatandaza mabomba yenye
urefu wa kilometa 141 sawa na asilimia 12.4.
Alisema mradi huo umelenga kunufaisha
vijiji 68 ambavyo 19 viko Kaskazini mwa Mto Wami na 49 Kusini.
Akizungumzia utendaji kazi wa mkandarasi
huyo, Mchomba alisema Serikali imechukua hatua za kimkataba kwa kumtoza gharama
ya kuchelewa kumaliza mradi kuanzia Februari 23.
“Pia mkandarasi amepewa notisi ya siku
100 kumtaka aongeze kasi ya kazi, vinginevyo tutasitisha mkataba ifikapo Mei 31
kulingana na kipengele namba 8.7 cha mkataba,” alisema.
0 comments:
Post a Comment