Mwandishi Wetu, Arusha
Laudit Mavugo |
BAO pekee lililofungwa dakika ya 54 na
mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo (pichani), limetosha kuipeleka Simba nusu
fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Madini FC katika mchezo
uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.
Kwa ushindi huo, Simba imeungana na
Mbao FC ya Mwanza kufuzu hatua hiyo ambayo juzi iliichapa Kagera Sugar mabao
2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Mbali na timu hizo, mabingwa watetezi
wa kombe hilo, Yanga itaumana na Prisons ya Mbeya na Azam FC itaoneshana jasho
na Ndanda FC katika kuwania kucheza hatua hiyo.
Katika mchezo huo, timu hizo zilianza
kwa kasi na kushambuliana kwa zamu ambapo katika dakika 15 za kwanza
zilionekana kusomana mchezo.
Dakika ya 22, Madini ilibisha hodi
langoni mwa Simba lakini shuti lililopigwa na Razaro Costantine dakika ya 22
liliokolewa na kipa, Daniel Agyei.
Simba ilijibu shambulizi hilo dakika
ya 30 kupitia kwa Ibrahim Ajibu ambaye alipiga shuti na mpira kugonga mtamba wa
panya na kurudi uwanjani lakini mabeki waliondosha hatari.
Timu hizo ziliendelea kuchezeana ubabe
ambapo katika kipindi hicho wachezaji wa Simba, Mzamiru Yassin na Juuko Murshid
walioneshwa kadi za njano na kwa Madini ni Awesu Awesu.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na
Simba kufanya shambulizi la nguvu dakika ya 46 kupitia kwa Ajib lakini kipa Cheramanda
aliudaka mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo.
Simba iliongeza presha langoni mwa
Madini na dakika ya 54, Mavugo aliifungia timu yake bao pekee kwa kichwa baada
ya beki, Hamis Hamis kuzembea kuondosha hatari langoni mwake.
Timu hiyo iliendelea kutakata ambapo
Winga Shiza Kichuya alikosa bao akibaki na kipa Cheramanda baada ya shuti lake
kuokolewa na beki Hamis kuondosha hatari.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Madini
iliendelea kujitutumua hasa alipoingia mshambuliaji mkongwe, Bakari Kigodeko
ambaye alionekana kuleta uhai katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Baada ya kipyenga cha mwisho
kupulizwa, mashabiki wa Simba walishangilia kwa nguvu na baadaye walionekana
wakitaka kuingia uwanjani lakini Polisi walifanya kazi ya ziada kuwazuia hivyo
walijikuta wakimfuata Mavugo kwa nyuma.
Simba: Daniel
Agyei, Besala Bukungu, Mohamed Zimbwe, Abdi Banda, Juuko Murshid, James Kotei,
Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin/ Jonas Mkude, Laudit Mavugo, Ibrahim
Ajibu/Athanas Pastory na Mohamed Ibrahim.
0 comments:
Post a Comment