Mwandishi Wetu
KAMPUNI za
ujenzi nchini zimeshauriwa kuungana na kushirikiana na za China ili kujifunza
namna wanavyofanya kazi kwa ufanisi.
Rai hiyo ilitolewa
jana Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Asasi ya Ushirikiano kati ya Tanzania na
China, Joseph Kahama, akisema kampuni za ujenzi nchini bado zina safari ndefu ya
kuongeza ujuzi na mbinu za kibiashara.
“Kujifunza kuna
njia nyingi ni utaratibu mzuri kujipanga kibiashara kwani ni muhimu kuelewa
kwamba zaidi ya asilimia 80 ya kampuni kubwa za ujenzi duniani zinatoka China,
na nchini zipo nyingi kwa sasa, hivyo huu ndio wakati wetu wa kuchota ujuzi,”
alisema Kahama.
Alifafanua,
kwamba Wachina ndio wanaongoza katika ujenzi duniani na mataifa mbalimbali yaliyoendelea kampuni za kichina ndizo
zilizosimamia majengo yao, hivyo kampuni za nchini haziwezi kukwepa zikitaka
kufanikiwa wajipenyeze na kuomba ushirikiano kwa Wachina na watajifunza mengi.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC East
Africa Limited), Yigao Jiang alisema kampuni yake imekuwa nchini tangu miaka ya
60 na wako tayari kusaidia Watanzania katika nyanja zote yakiwamo masuala ya
kijamii.
“Mbali ya
kushiriki ujenzi wa magorofa na miundombinu, kampuni yetu inaguswa na matatizo
ya kijamii kwa sababu Watanzania ni ndugu zetu sasa, tumeshiriki ujenzi wa reli
ya Tazara, tumejenga jengo la Ushirika (Mnazi Mmoja), tumejenga jengo la Nasaco
(Dar es Salaam).
Alisema: “Vilevile
jengo la ukumbi mpya Ikulu, Dar es Salaam tumeshiriki kuujenga na sasa
tunajenga makutano ya barabara za juu Ubungo.”
Kuhusu fursa
zinazopatikana kutokana na kampuni za ujenzi za China, Kahama alisema:
“Watanzania wanapata ajira kwa sababu wasimamizi ni Wachina, lakini wafanyakazi
wanatoka hapahapa, vilevile wananunua mchanga, saruji, kokoto, nondo na vifaa
vingine vya ujenzi nchini.
0 comments:
Post a Comment