Mwandishi Wetu
Profesa Sospeter Muhongo |
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amezindua
Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu mkoani Pwani akisema mkoa huo
utapewa kipaumbele kwa kuwa ni kimbilio la wawekezaji na ukanda wa viwanda.
Aidha, ametaka Watanzania kuacha kujidharau kupitia mradi huo kwa
kuwa ni mkombozi wao kwani mwaka 2007 kulikuwa na asilimia mbili pekee ya
watumiaji nishati ya umeme lakini sasa kasi imefikia asilimia 49.5.
Akizindua mradi huo juzi na kumtambulisha mkandarasi kutoka Tunisia
kampuni ya Steg, alisema ni wakati wa kuchangamkia fursa hiyo kwa kila
Mtanzania mwenye mahitaji ya umeme.
Alisema katika awamu hiyo, zimetengwa Sh trilioni moja ambapo
vijiji 3,559 vitafikiwa nchini huku Pwani ikifikiwa vijiji 150 vilivyokuwa
havijafikiwa na awamu ya kwanza na ya pili.
Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanafikia vijiji vyote 12,268 nchini,
kwa umeme wa Tanesco ili kila mmoja anufaike nao na kuondokana na vibatari.
Profesa Muhongo alisema wakati mradi huo wa REA ukianza katika maeneo
mbalimbali nchini ni lazima upelekwe katika zahanati, shule na vituo vya dini.
Alisema mkoa wa Pwani ni kati ya iliyojikita kwenye viwanda na
uwekezaji hivyo ni lazima nguvu kubwa ielekezwe huko.
Profesa Muhongo aliutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kuweka tayari
wataalamu wake na wa Tanesco, REA, wabunge na Meneja wa Kanda, ili kubainisha
mahitaji yatakayorahisisha kufanyiwa kazi na wizara.
Alisema fedha zilizotengwa ambazo ni karibu Sh trilioni moja
zilizotengwa kwa ajili ya mradi huohazitakuwa sehemu ya fidia kwa ajili ya
maeneo ambayo umeme huo utapita.
Aliupongeza uongozi wa mkoa wa Pwani, kwa kukuza sekta ya viwanda
na uwekezaji, pamoja na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wa Kibaha
Vijijini, Hamoud Jumaa kwa kupigania maendeleo ya majimbo yao.
Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo alisema mkoa huo unakabiliwa na
changamoto ya wateja na kuomba uongezwe nguvu ya umeme wa megawati 60 ambapo
kwa sasa unapata megawati 38 hadi 40 ambazo hazikidhi mahitaji ikizingatiwa kuwa
mkoa unasheheni viwanda.
Ridhiwani alieleza mahitaji ya umeme kuwa ni makubwa kwenye vijiji
vya Chalinze na kuomba mahitaji mapya yaingizwe kwenye bajeti kwa lengo la
kufanyiwa kazi katika bajeti ya mwaka 2017/18.
0 comments:
Post a Comment