Suleiman Msuya
MKURUGENZI Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) kwa
Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia, Bella Bird amezindua mradi wa kuzalisha
umeme kwenye maporomoko ya Mto Rusumo ambao utatoa megawati 80 kwa nchi tatu
Afrika Mashariki.
Bird alizindua chanzo hicho cha umeme
jana katika eneo la Rusumo ambapo mawaziri wa sekta hiyo kutoka nchi wanufaika;
Rwanda, Burundi na Tanzania walishiriki.
Alisema mradi huo ni moja ya mikubwa
katika ukanda huo na anaamini utachochea kuinua uchumi, ajira na maendeleo kwa
nchi husika.
Mkurugenzi huyo alisema mradi huo umeonesha
umuhimu wa ushirikiano wa nchi husika kwani utagusa maisha ya wananchi moja kwa
moja na kukuza uchumi.
“Mfano mradi ukikamilika utasaidia
wanawake wanaokutana na ukatili, kuongeza uzalishaji, kuinua shughuli za kilimo
na mawasiliano ya aina mbalimbali,” alisema.
Bird alisema Tanzania, Burundi na Rwanda
zitakuza familia zao ambapo kila nchi itapata mgao kulingana na hitaji la
makazi.
“Burundi watapata megawati 27 hivyo kuongeza
asilimia 50 ya hitaji la umeme na itapunguza gharama ya kununua uniti moja kwa
senti nne tofauti na za sasa ni senti 10 kwa uniti moja,” alisema.
Alisema Rwanda gharama ya kununua umeme
ni senti 26 na Tanzania senti 12 hivyo itakuwa mkombozi katika maeneo husika na
kuchochea maendeleo.
Alisema hakuna shaka kuwa uwepo wa umeme
ni moja ya vitu ambavyo vinachochea maendeleo, kwani jamii imekuwa ikililia
hitaji hilo kila uchwao ili kuendeleza biashara zao.
”Umeme unatengeneza ajira, matumaini,
kujiamini na inajulikana kuwa katika kufikia maendeleo chanzo sahihi ni uwepo
wa umeme wa uhakika,” alisema.
Alisema hiyo ni moja ya jitihada za ukanda
wa Maziwa Makuu kutekeleza mikakati ambayo imewekwa na Umoja wa Mataifa (UN), kupitia
aliyekuwa Katibu Mkuu, Ban Ki-moon na Rais wa WB, Dk Jim Yong Kim miaka minne
iliyopita ili kuendelea.
Bird alisema katika kipindi hicho, WB
ilikubali kutoa dola za Marekani bilioni 1.3 ambapo hadi sasa imetoa dola
bilioni 1 za Marekani.
Mkurugenzi mkazi huyo alisema matarajio
yao ni kuona mradi huo unakamilika kwa wakati ifikapo 2019 na kwamba wao
wamefanya kinachowahusu.
Alisema katika kutekeleza miradi yao pia
wanashirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) hivyo wanawashukuru kwa
ushirikiano wao.
0 comments:
Post a Comment