Mwandishi Wetu
Jordan Rugimbana |
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amezikumbusha taasisi za
elimu ya juu nchini
kuhakikisha zinaongeza uwezo wa madawati ya mikopo yaliyopo katika
taasisi zao ili yaweze kutoa ushirikiano unaotakiwa kutatua changamoto za
utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Mkuu wa mkoa huyo alitoa agizo hilo jana, wakati akifungua mkutano
wa kazi wa siku mbili wa watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB), na maofisa mikopo zaidi ya 100 kutoka taasisi za elimu ya juu
nchini wanaokutana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Majukumu ya bodi ni mazito na hivyo, inahitaji ushirikiano wa kutosha
kutoka kwa wadau mbalimbali mkiwemo maofisa mikopo mliopo vyuoni na mnaokutana na
wanafunzi kila siku,” alisema Rugimbana, katika hotuba yake iliyosomwa kwa
niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Dodoma, Gosbert Damazo.
Akizungumza katika mkutano huo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi,
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema bodi yake inatambua
mchango mkubwa unaotolewa na maofisa mikopo hao katika kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waliopo katika taasisi
mbalimbali.
“Maofisa hawa ndiyo wanaotuunganisha na wanafunzi katika utendaji
kazi wetu wa kila siku, hivyo ni watu muhimu sana kwetu na tunathamini sana
mchango wao na wa taasisi zao,” alisema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, bodi yake itatumia mkutano huo wa siku mbili
kuwakumbusha maofisa hao wajibu wao katika kutunza kumbukumbu muhimu za wanufaika
wa mikopo na majukumu yao muhimu ili kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza
malalamiko ya wadau wakiwemo wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Mkurugenzi mtendaji huyo alikumbusha kuwa, mwaka 2011, serikali
ilivielekeza vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kuanzisha madawati ya mikopo ya
elimu ya juu ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu
inayotolewa na serikali.
“Tangu mwaka 2011, kumekuwa na mafanikio makubwa katika utendaji
wetu kutokana na kuongezeka kwa ufanisi. Hivi sasa malalamiko kutoka kwa
wanafunzi
yamepungua sana,” alisema Badru.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Taaluma), Profesa Lawrence
Msoffe ambaye alihudhuria hafla ya ufunguzi, alisema mkutano huo ni muhimu kwa
kuwa utaisaidia bodi kupata mrejesho kutoka kwa maofisa hao ambao ndiyo
wanaosimamia masuala ya utoaji mikopo katika vyuo kila siku.
HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi
rasmi Julai 2005, pamoja na mambo mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa
wanafunzi Watanzania wasio na uwezo na kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na
serikali kuanzia mwaka 1994/1995.
0 comments:
Post a Comment