Makamba alia na mazingira nchini


Abraham Ntambara

Januari Makamba
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba, amesema hali ya mazingira nchini si nzuri kutokana na ulegevu wa muda mrefu wa kusimamia sheria za uhifadhi.

Makamba alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam baada ya ufunguzi wa mkutano wa siku tatu ulioandaliwa na Korea kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) ambao utazungumzia maendeleo endelevu kwa kutumia teknolojia inayozingatia hifadhi ya mazingira.

“Hali si nzuri kusema ukweli, kumekuwa na ulegevu wa muda mrefu katika kusimamia sheria ya uhifadhi wa mazingira, sasa hivi kidogo tunaamka na kuongeza kasi na ukali zaidi ili kulinda mazingira,” alisema Makamba.

Alisema hayo yanafanyika ili kuhakikisha mito na vyanzo vya maji haviharibiwi, misitu inahifadhiwa na viwanda havimwagi sumu na kutoa moshi ambapo alieleza kuwa kwa sasa pia watu wanafanya tathmini ya athari kwa mazingira kutokana na shughuli zao za uchumi.

Alisema kuelekea ujenzi wa viwanda ni vema kuweka hali ya mazingira vizuri hivi sasa ambapo kuna dhana miongoni mwa jamii kuwa tujenge kwanza na suala la mazingira litashughulikiwa baadaye.

Aliongeza kuwa anaamini mkakati wa ujenzi wa viwanda nchini utakwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira, kutokana na kwamba nchi zenye viwanda zimekuwa zinaathiriwa na uchafuzi wa mazingira.

Makamba alisema Korea ni nchi ya mfano inayoonesha kuwa pamoja na maendeleo ya viwanda, uhifadhi wa mazingira pia unawezekana.

Mkutano huo unajumuisha wataalamu, wasomi na wakuu wa taasisi duniani zinazoshughulika na maendeleo na mazingira.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo