Na Malisa Godlisten
KWA muda
wa miezi kadhaa sasa kumekuwa na changamoto ya kisiasa kati ya chama tawala,
vyama vya upinzani, jeshi la polisi na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.
Changamoto
hiyo inatokana na hali ya sintofahamu iliyoibuka juu ya utendaji na shughuli za
vyama vya siasa nchini. Mgogoro huu ulianza baaada ya Rais John Pombe Magufuli
kupiga marufuku mikutano ya kisiasa na maandamano akitaka wananchi na wafuasi
wa vyama vya siasa kujiegemeza zaidi katika shughuli za maendeleo badala ya mikutanoi
ya kisiasa au maandamano.
Agizo
hili la Rais lilipokelewa na vyombo vya dola ambapo Jeshi la Polisi lilipiga
marufuku mikutano ya kisiasa, maandamano hata vikao vya ndani kwa madai kuwa
shughuli za kisiasa ni hadi mwaka 20120. Chama cha Demokrasi na maendeleo
(CHADEMA) na vyama vingine vinavyounda UKAWA vikajikuta vimekua wahanga wa
kwanza wa agizo hilo. Walizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani
wala semina na vikao kazi vya chama.
Wakati
vyama vya upinzani vikizuiwa kufanya shughuli zao za kisiasa, Chama Cha
Mapinduzi kinaendelea na shughuli zake ikiwa ni pamoja na Rais Magufuli kutumia
mikutano mbalimbali ya hadhara kukinadi chama chake. Bila shaka hili ndilo
linalofanya vyama vya upinzani kuona kuwa wanafanyiwa uonevu lakini chama cha
mapinduzi kinapendelewa.
Tume
hiyo iliandaa mkutano utakaohusisha taasisi sita, ikiwamo Jeshi la Polisi
lililozuia mikutano, CCM inayoendesha Serikali na Chadema inayopinga maamuzi ya
Serikali kwa madai kuwa yanakandamiza demokrasia na kukiuka misingi ya utawala
bora.
Waliopaswa
kuhudhuria kikao hicho ni makatibu wakuu wa vyama hivyo, Abdulrahman Kinana
(CCM), Vincent Mashinji (Chadema) na Ernest Mangu (Mkuu wa Jeshi la Polisi),
Jaji Francis Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa), George Masaju (Mwanasheria
Mkuu wa Serikali) na Katibu mkuu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Mkutano huo uliitishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga ambapo
ulipaswa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Kisheria
Tume ya Haki na Utawala Bora ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za
binadamu, kuchunguza jambo lolote, kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo vingine
vya umma na kuchukua hatua za kukuza, kuendeleza, usuluhishi na suluhu miongoni
mwa watu na taasisi.
Lakini
katika hali ya kushangaza Chama cha mapinduzi (CCM), Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP) na Mwanasheria Mkuu (AG) hawakutokea kuhudhuria mkutano huo wa usuluhishi
ulioitishwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kumaliza mvutano
ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chadema.
Hatua
hii ya vyombo vya dola pamoja na CCM kushindwa kuhudhuria mkutano huo ni dalili
kuwa hawako tayari kutafuta utatuzi wa mgogoro huo. Hii inaweza kuwa hatua
mbaya katika ukuaji wa demokrasia nchini.
Jeshi la
Polisi limekuwa likijinasibu kila mara kuwa ni walinzi wa usalama wa raia na
mali zao. Sasa mbona wanaona dalili za usalama wa raia kuharibika na hawataki
kuchukua hatua? Au wanasubiri hadi September mosi ndipo waanze kuchukua hatua?
Kwa nini Polisi hawataki kuzuia mgogoro (proactive) badala yake wanataka
mgogogro utokee ndipo wahangaike kuutatua (reactive)? Polisi wamekuwa wakizuia
matukio mbalimbali ya kijamii kwa taarifa za kiitelijensia. Je hawajapata
taarifa za kiintelijensia kuwa Septemba mosi hali ya usalama inaweza kuzorota
kama wasipochukua hatua? Sasa kwa nini wamekataa kushiriki katika mkutano wa
usuluhishi? Wanapenda kuona mgogoro huu ukiendelea? Ikiwa CHADEMA pekee ndio
waliotuma uwakilishi katika mkutano huo wa usuluhishi, ina maana kuwa ni
CHADEMA pekee wenye dahamira ya kweli ya kutafuta suluhu ya mgogoro huu. Je CCM
Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwanasheria mkuu ambao ni wadau wakuu wa mgogoro
huu hawataki kuona mgogoro huu ukiisha? Kitendo cha kutohudhuria mkutano wa
usuluhishi ni dalili kuwa kuna agizo lililowazuia kushiriki. Haiwezi kuwa
bahati mbaya. Bila kukutana hakuna lolote linaloweza kufanyika ili kutafuta
suluhu. Wataalamu wa utatuzi wa migogoro wanaeleza kuwa ikiwa pande
zinazozozana zimekubali kukutana ni dalili nzuri ya kutafuta suluhu. Upande
usiokubali kushiriki hauko tayari kuona mgogoro ukimalizwa. Hii ni kusema
kwamba CCM, IGP na AG hawapo tayari kumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo. Hii
haiwezi kuwa habari nzuri katika mchakato wa ukuaji wa demokrasia nchini. Na ni
aibu kwa chama tawala na taasisi nyeti kama jeshi la polisi na ofisi ya mwanasheria
mkuu kukataa kushiriki katika mkutano wa usuluhishi.
0 comments:
Post a Comment