Saed Kubenea |
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea
(Chadema) amefikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya
saa 2, kutokana na tuhuma za kuandika makala ya uchochezi kwenye gazeti la
Mwana Halisi Julai 25 na 31.
Aidha, Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa
Mbaruku (CUF) aliyekamatwa juzi saa nne asubuhi kwa madai ya uchochezi alihojiwa
na kuachiwa kwa dhamana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, baada
ya Kubenea kuhojiwa, Wakili wake, Tundu Lissu alisema Polisi ilimwita kwa
mahojiano kuhusu makala hayo yaliyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu Zanzibar,
ambapo kwa mujibu wa Jeshi hilo, ni ya kichochezi.
Alisema katika mahojiano hayo Kubenea
alitakiwa kuelezea watu aliodai waliteswa kama alionana nao na kuwasiliana na
Polisi na kwamba asilimia kubwa ya maswali hayo yalihusu makala hiyo.
Alisema Kubenea aliachiwa kwa dhamana
ya Polisi na kutakiwa kuripoti Agosti 18, kwa hatua nyingine za kipolisi.
Wakili alisema jitihada zinazofanywa na Serikali na Jeshi hilo ni
kuwanyamazisha lakini hazitafanikiwa kwani dhamira yao ni kupigania haki,
sheria na kulinda Katiba ya nchi na si vinginevyo.
Naye Ibrahim Kunoga anaripoti kutoka
Tanga, kwamba Polisi wilaya ya Tanga, imemwachia kwa dhamana ya Sh milioni 20
Mbunge Mbaruku aliyekamatwa kwa madai ya kufanya mikutano ya hadhara na kutoa
maneno ya uchochezi na yanayoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari
baada ya kupewa dhamana, Mbunge huyo alisema kilichofanywa na Polisi ni
mwendelezo wa uminyaji haki ya demokrasia ili viongozi wakose uhuru wa
kuzungumza na wananchi.
Mbaruku alisema Jeshi hilo lilimtaka
asiendelee na mikutano ya hadhara, asitoke nje ya Tanga na kuzuiwa hati yake ya
kusafiria. Alisema CUF itaendeleea kupinga hatua hiyo ya Polisi ili kufikisha
ujumbe kwa wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
Mwenyekiti CUF wa Wilaya, Rashid Jumbe
alilaani kitendo cha Jeshi hilo kumkamata mbunge huyo ambaye alikuwa
akitekeleza majukumu ya kawaida ya kichama na kufikisha ujumbe kwa wananchi wake.
Jumbe alisema wataendelea kumwunga
mkono ili kuhakikisha haki inatendeka na kuwataka wananchi wa Tanga pia
kumwunga mkono pamoja na chama ili kufikisha dhamira nzuri ya kutekeleza
majukumu ya kichama.
0 comments:
Post a Comment